2013-10-21 07:58:57

Sinodi maalum kuhusu Familia hapo 2014 inapania kuangalia changamoto za familia katika shughuli za kichungaji!


Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Bikira Maria katika Mwaka wa Imani, amewataka wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, wanamwilisha maneno makuu matatu katika maisha yao ya kila siku: Maneno haya ni: Tafadhali, Sahamani na Asante. RealAudioMP3

“Changamoto za familia kichungaji katika Uinjilishaji” ndiyo kauli mbiu itakayoongoza Maadhimisho ya Sinodi Maalum kwa ajili ya familia, itakayofanyika kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba, 2014.

Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kwa kutangaza Maadhimisho ya Sinodi Maalum kwa Ajili ya Familia mwezi Oktoba 2014 inapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu dhamana n anafasi ya familia katika maisha na utume wa Kanisa. Huu utakuwa ni muda muafaka wa Kanisa kama Jumuiya ya waamini kusali na kufanya tafakari ya kina kuhusu familia.

Hii ni Sinodi itakayowahusisha viongozi wakuu wa Kanisa pamoja na wajumbe kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Ni ufafanuzi uliotolewa hivi karibuni na Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican wakati akifafanua kwa kina, uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuitisha Sinodi Maalum kwa ajili ya Familia, taasisi ambayo ni msingi wa Kanisa na Jamii, lakini inayokabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wake.

Padre Federico Lombardi anasema, huu ni mwelekeo sahihi kwamba, Kanisa, liweze kutembea kwa pamoja katika mikakati ya kichungaji mintarafu utume na maisha ya familia, chini ya usimamizi na uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro akisaidiana na Maaskofu wenzake katika kutekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Sinodi itagusia mambo msingi yanayopaswa kushughulikiwa na Kanisa katika ujumla wake.

Ufumbuzi wa changamoto na fursa mbali mbali kuhusu utume na maisha ya familia utaendelea kutekelezwa na wadau mbali mbali kila mtu kadiri ya wajibu na dhamana yake, ili kuondokana na mkanganyiko unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa mafundisho ya Kanisa kuhusu familia. Lengo la Baba Mtakatifu Francisko ni kuhakikisha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu pamoja na Makanisa mahalia yanashikamana katika kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya familia.









All the contents on this site are copyrighted ©.