2013-10-21 08:53:17

Mshikamano wa Papa kwa watu waliokumbwa na janga la moto nchini Australia


Baba Mtakatifu Francisko amewatumia Maaskofu Katoliki nchini Australia ujumbe wa mshikamano wa dhati kutokana na janga la moto uliosababisha maafa makubwa Kusini mwa nchi hiyo. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Pietro Parolin, Katibu mkuu mpya wa Vatican.

Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wote waliopoteza maisha; wale ambao nyumba zao zimeungua na maeneo ya kazi kuharibiwa vibaya, bila kuwasahau wote waliojiunga na kikosi cha zima moto ili kunusuru maisha na mali ya watu. Baba Mtakatifu anapenda pia kuchukua fursa hii kuwafariji wagonjwa na kwamba, anawaombea wote na kuwapatia baraka zake za kitume.

Huu ni ujumbe wa kwanza kabisa kuandikwa na Askofu mkuu Pietro Parolin tangu alipochaguliwa na hatimaye kuanza utume wake kama Katibu mkuu wa Vatican baada ya Kardinali Tarcisio Bertone, kuhitimisha muda wake wa uongozi kama Katibu mkuu wa Vatican, utume ambao aliufanya kwa takribani miaka saba.







All the contents on this site are copyrighted ©.