Makanisa na mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani duniani
Jumuiya za Kikristo zinapaswa kujikita katika kulinda, kutetea na kudumisha misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli.
Hii ni changamoto
iliyotolewa hivi karibuni na Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa
Ulimwenguni, wakati alipokuwa anahuhudhuria Kongamano la Kimataifa lililokuwa limeandaliwa
na Baraza la Kipapa la Haki na Amani kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 tangu
Papa Yohane XXIII alipochapisha Waraka wa Kichungaji, Pacem In Terris, Amani Duniani.
Dr. Tveit anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa
kweli ni mahujaji wa kiekumene katika mchakato wa kulinda na kudumisha haki na amani
duniani, kwa kutambua kwamba, Makanisa yanashiriki kwa namna ya pekee katika mpango
wa Mungu wa kulinda na kudumisha haki na amani.
Makanisa sehemu mbali mbali
za dunia yanaendelea kulaani na kukemea vita na migogoro inayofuka moshi na kuendelea
kusababisha maafa na majanga makubwa miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Waamini na
watu wenye mapenzi mema, wanapaswa kuendelea kuzishinikiza Serikali na viongozi wao,
ili kuhakikisha kwamba: haki, amani na utulivu vinapatikana kwa wote na kwamba, kama
viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao
ya wengi.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linajiandaa kuadhimisha Mkutano Mkuu
wa Kumi, unaoongozwa na kauli mbiu “Mungu wa maisha, tuongoze katika haki na amani”
Mkutano huu unatarajiwa kufunguliwa rasmi hapo tarehe 30 Oktoba hadi tarehe 8 Novemba
2013, huko Busan, Korea ya Kusini. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza
juhudi za upatanisho kwa Korea zote mbili, kwa kutambua kwamba, amani ni msingi mkuu
wa maisha, unaoonesha upendo wa Mungu kwa binadamu wote.
Dr. Tveit anasema,
amani bado iko mashakani huko Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi Barani Asia
kama vile Pakistan. Wakristo ambao wanaonekana kuwa ni kundi dogo katika nchi kama
hizi, nao pia wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa dhidi ya watu wenye imani na itikadi
kali za kidini, wanaohatarisha usalama wa maisha ya raia wengine, kama kwamba, wao
ni “wananchi wa kuja”.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaendelea kutoa changamoto
kwa Makanisa sehemu mbali mbali za dunia kuhakikisha kwamba, kwa pamoja wanatolea
ushuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho; daima wakisimama kidete kulinda,
kutetea na kutunza mazingira kwani hii ni sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu
amekabidhiwa kuilinda na kuitunza.