Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja
wa Mataifa, FAO anasema, dunia ina uwezo mkubwa wa kuweza kuzalisha chakula kinachoweza
kutosheleza mahitaji ya binadamu wote, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba,
baa la njaa na utapiamlo limekuwa ni janga kwa mamillioni ya watu duniani, jambo ambalo
kimsingi ni kashfa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kuna haja
kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha utamadhuni wa mshikamano wa dhati ili
wale waliobahatika kupata neema na Baraka ya kuwa na chakula kingi waweze kugawana
na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Inasikitisha na kuhuzunika kusikia na kushuhudia
watu wakitafuta makombo ya chakula kilichotupwa jalalani! Ni changamoto hizi ambazo
Baba Mtakatifu Francisko alizotoa alipokutana na wajumbe wa FAO walipomtembelea mjini
Vatican hapo tarehe 30 Juni 2013.
Historia inaonesha kwamba, ushirikiano wa
dhati kati ya wakulima, wafugaji, wanasayansi na wahandisi, wamefanikiwa kuhakikisha
kwamba, kunakuwepo na uzalishaji wa chakula cha kutosha kutokana na ongezeko la idadi
ya watu wa duniani. Tangu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, idadi ya atu imeongezeka
maradufu, lakini uzalishaji wa chakula umeongezeka kwa asilimia 40% . Haya ni mafanikio
makubwa katika mapambazo ya Karne ya 21. Lakini ongezeko hili la uzalishaji wa chakula
linakwenda sanjari na utupaji mkubwa wa chakula ambacho kingetumika kwa ajili ya kuganga
njaa kwa watu wanaoendelea kutumbukia katika janga la njaa duniani.
Maendeleo
ya sayansi na teknolojia yamechangia kwa namna ya pekee kuchakaa kwa ardhi kutokana
na uwepo wa matumizi mabaya ya ardhi, maji na misitu. Mambo haya yamepelekea pia kupungua
kwa uwepo wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Kuna makundi makubwa ya watu yanalazimika
kuyakimbia makazi nan chi zao kutokana na baa la njaa na watoto wengi wanaendelea
kupoteza maisha kutokana na utapia mlo wa kutisha. Kutokana na kilio kama hiki, kuna
haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaibua mbinu mkakati utakaoweza
kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula kwa sasa na kwa vizazi vijavyo, sanjari na
kuhakikisha kwamba, watu million 870 wanaokabiliwa na baa la njaa kwa sasa wanapata
chakula.
Bwana Graziano da Silva anabainisha kwamba, idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa
na baa la njaa wanaishi katika nchi zinazoendelea duniani. Janga la njaa linaanza
kupiga hodi kwa kasi hata katika nchi tajiri kutokana na athari za myumbo wa uchumi
kimataifa. Baa la njaa linapukutisha maisha na matumaini ya maisha kwa mamillioni
ya watu duniani. Dhana ya uhakika wa usalama wa chakula inapania kuhakikisha kwamba,
kila mtu anakuwa na uhakika wa chakula ili aweze kupata maisha bora na endelevu.
Anasema,
katika makala aliyoiandika kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano, linalotolewa na
Vatican kila siku kwamba, Kanisa limewekeza kwa kiasi kikubwa katika masuala ya afya
ya mwanadamu, kama ilivyo pia kwa dini mbali mbali duniani. Lakini, bado kuna watu
ambao wanashinda na kulala njaa kwa kukosa chakula, changamoto kwa waamini wa dini
na madhehebu mbali mbali duniani kujenga na kuimarisha utamaduni wa upendo na mshikamano
kwa jirani zao, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; watu wanaopaswa kuonjeshwa
upendo kadiri ya Maandiko na Misaafu mitakatifu.
Inasikitisha kuona kwamba,
ubinafsi, uchoyo na tamaa ya fedha vinaendelea kuwa ni kizingiti katika mchakato wa
kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani, kiasi cha dunia kuendelea kushuhudia
mamillioni ya watu wakiteseka na kufariki dunia kutokana na baa la njaa na utapia
mlo wa kutisha. Kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, njaa haiwezi kupatiwa ufumbuzi
na kwamba, hii eti ni sehemu ya maisha ya binadamu, jambo ambalo linapingwa vikali
na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula
Duniani kwa Mwaka 2013.
Baa la njaa na utapiamlo ni matokeo ya umaskini wa
hali na kipato unaokwamisha jitihada za familia nyingi kujijengea uwezo wa kununua
au kuzalisha chakula bora na cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia zao. Baa
la njaa linakwamisha mchakato wa maendeleo endelevu kwani hakuna hata siku moja mtu
mwenye njaa atakayeweza kuzalisha kwa wingi au kusoma, akaelewa na kuhamasika zaidi.
Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanapata fursa ya kupata chakula kwani
chakula cha kutosha kipo!
Watu watambue kwamba, chakula ni haki ya kila mtu!
Mapambano dhidi ya baa la njaa ni jambo linalowashirikisha wadau mbali mbali na wala
si kwa ajili ya Serikali pekee! Kila mtu atekeleze wajibu na dhamana yake, hapo baa
la njaa litaweza kufutika kama ndoto ya mchana! Jamii ijenge ushirikiano wenye tija
na utengamano; mshikamano unaojali na kuwajibisha kwa kuwashirikisha wakulima wadogo
wadogo na wanawake kuchangia katika mchakato wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula
kimataifa. Brazil imeweza kufuta baa la njaa, jambo hili pia linawezekana kwa nchi
nyingine duniani!
Wakulima wadodo wakiwezeshwa pamoja na mpango wa chakula
kwa wanafunzi wa shule za msingi ni mikakati inayoweza kuboresha maisha ya wananchi
wengi duniani sanjari na kupunguza vifo vya watoto wachanga kutokana na utapiamlo
wa kutisha. Watoto wa shule watahamasika kusoma zaidi na nguvu kazi itaendelea kufaidi
matunda ya jasho lake, kumbe, kilio cha maboresho ya uhakika wa usalama wa chakula
duniani anasema, Bwana Josè da Silva una faida kubwa kwa Jamii husika na maendeleo
ya wengi.
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujenga utamaduni wa kuhifadhi chakula
kwani chakula kingi kinachozalishwa kinapotea tangu wakati mazao yakiwa shambani hadi
pale yanapowafikia walaji. Watu wanamwaga chakula kingi, chakula ambacho kingeweza
kutumika kwa ajili ya maskini. Jamii ijifunze kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza
mazingira ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabia nchi. Wazazi pia wawajengee
watoto wao tabia ya kula vyema na chakula bora. Wasiridhike kuwaona watoto wamenenepa
na kuwa na vitambi, wakadhani kwamba, huo ndiyo ustaharabu wa ulimwengu mamboleo!
Bwana
Graziano da Silva Mkurugenzi mkuu wa FAO anasema, Serikali kwa sasa zihakikishe kwamba,
wananchi wao wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula ili waweze kuchangia katika
ustawi na maendeleo yao. Kila mdau akitekeleza wajibu wake, baa la njaa linaweza kupewa
kisogo duniani!
Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.