2013-10-21 10:06:46

China kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii nchini Tanzania


China imeahidi kuleta nchini Tanzania watalii 30,000 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani. Ahadi hiyo imetolewa Jumapili, Oktoba 20, 2013 na Mwenyekiti wa Wakala wa kutoa huduma za usafiri wa China na Hong Kong (China Travel Services - Hong Kong Limited - CTS) Bw. Zhang Xuewu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jijini Shenzen, China.

Alisema kampuni yake itawandaa mawakala wa usafirishaji watalii ili kuhakikisha kuwa watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuja Tanzania. “Wengi wanapenda kutembelea mbuga, lakini hapa nchini wamezoea kuona walio sakafuni, wakija watawaona wanyama live” (akimaanisha kuwa Wachina wamezoea kuona wanyama wa sanamu kwenye makumbusho yao hapa jiji la Shenzen).

Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China alisema haelewi ni kwa nini kampuni hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za Afrika Mashariki wakati haina urafiki nazo lakini imeshindwa kuwaleta Tanzania kwenye ambayo ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu.

Akizungumza na Bw. Xuewu pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu alisema amepewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kufuatilia suala la watalii wa kutoka China hasa ikizingatiwa kwamba mazungumzo ya jambo hili yalianza wakati wa Rais wa awamu ya tatu, Ndugu Benjamin Mkapa.

“Katika bara la Afrika hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania. Na tovuti ya www.safaribooking.com imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayofaa kwa safari za mbugani kama mtu anataka kuona vivutio vizuri na vya asili. Sasa ni kwa nini hatupati watalii wa kutosha na tunafanyaje ili kubadilisha hali hiyo?,” alihoji.

Alisema njia mojawapo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na ndege ya moja moja kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam jambo alisema litasadia kupuinguza kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara mbili hadi tatu ili kufika Tanzania. “Tuangalie uwezekano wa kuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi Dar es Salaam au Arusha... wenzetu Kenya na Afrika Kusini wameweza kupata watalii wengi sababu wana ndege za moja kwa moja,” alisema.

Alimshawishi Mwenyekiti huyo aangalie pia uwezekano wa kujenga mahoteli katika mikoa ya Tanzania ili kupunguza uhaba wa vyumba punde watalii wakianza kufurika. Pia alimhakikishia fursa ya kujenga uwanja wa gofu chini ya mlima Kilimanjaro kwani yote mawili ni maeneo ambayo kampuni yake inao uwezo wa kufanya kama sehemu ya majukumu yake.

Pia alimpa wazo kwamba kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya urafiki baina ya Tanzania na China, CTS inaweza kuandaa kundi kubwa la wakala wakaja Arusha na kufanya mkutano wa siku mbili au tatu na kisha wakapata fursa ya kujadili namna ambavyo Tanzania na China zinaweza kushirikiana kukuza suala la utalii. “Mkimaliza mkutano wenu mnasaini makubaliano baina yenu na Bodi ya Utalii, mambo yanasonga mbele,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bw. Xuewu alikiri kuwepo kwa mazungumzo ya wakuu wa nchi akisema: “Mwaka 2004, Rais Hu Jintao alifikia makubaliano na Rais (Benjamin) Mkapa kwamba watafungua milango ya utalii kwa Tanzania. Mwezi Machi, 2013, Rais Kikwete na Rais wa China, Bw. Xi Jinping walirudia tena mazungumzo hayo na kukubaliana kuwa Tanzania itapewa kipaumbele cha pekee kwa watalii wa kutoka China.

“Na hata wewe na Waziri Mkuu wetu, Bw. Li Keqiang, mwezi huu mmeshuhudia mawaziri wakisaini makubaliano kuhusiana na suala hilo, kwa kweli kama Serikali mmedhamiria kuhakikishia kuwa mnainua viwango vya utalii ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania,” alisema.

Alimshukuru Waziri Mkuu kwa wazo lake kuhusu mkutano na MoU na kumhakikishia kuwa wako tayari kujenga hoteli, viwanja vya gofu, kuanzisha tawi la kampuni yao ya uwakala kama ambavyo Waziri Mkuu amewasahauri.









All the contents on this site are copyrighted ©.