2013-10-19 12:40:50

Mwenyeheri Stefano Sàndor ni mfano wa uaminifu kwa wito wa Kikristo, majitoleo ya elimu kwa vijana na majiundo makini ya Kikristo!


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 19 Oktoba 2013, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Stefano Sàndor, mwamini mlei wa Shirika la Wafranciskani wa Sale kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye jimbo kuu la Budapest, nchini Hungaria.

Mwenyeheri Stefano Sàndor aliyeishi kati ya mwaka 1914 hadi mwaka 1953, alizaliwa na kuishi katika familia iliyokuwa imejikita katika misingi ya Kikristo. Ni mtu aliyeishi katika kipindi kigumu cha historia ya Hungaria. Daima alikuwa ni mwamini aliyependa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, katika Parokia iiliyokuwa inaongozwa na Ndugu wadogo wa Mtakatifu Francisko.

Tangu ujana wake, alitambua umuhimu wa dini na tunu msingi za maisha ya kibinadamu, mambo yaliyomfanya kujisikia kuwa na wito wa kujiunga na Wasalesiani wa Mtakatifu Bosco. Alijikita katika majiundo endelevu yaliyokuwa yanatolewa na Wasalesiani.

Madhulumu ya kidini nchini Hungaria kunako mwaka 1949, yalipelekea mali nyingi ya Kanisa kutaifishwa na waamini na watawa wakakumbana na "ufagio wa chuma", hali iliyowafanya wengi wao kukimbilia uhamishoni au kuishi katika hali ya uficho. Stefano naye akajikuta anaikimbia nchi yake kwa kuhofia usalama wa maisha yake anasema Kardinali Angelo Amato. Baadaye alipata ujasiri wa kuendelea kazi yake ya uchapishaji, ingawa alitambua kwamba, ilikuwa imepigwa rufuku na utawala wa kinazi.

Tarehe 28 Julai 1952, Polisi ikamtia pingu mikononi na kupelekwa gerezani, alikoteswa na kunyanyaswa kutokana na imani yake kwa Kristo na Kanisa lake. Akapandikiziwa mashitaka kwamba, alikuwa na mpango wa kutaka kuipindua serikali na hatima yake ni kuhukumiwa kifo, adhabu iliyotekelezwa hapo tarehe 8 Juni 1953. Kunako mwaka 1990 adhabu ya kifo aliyopewa Stefano ikafutwa na akapewa nishani maalum na Serikali ya Hungaria.

Mwenyeheri Stefano ameliachia Kanisa mambo makuu matatu: Uaminifu kwa maisha na wito wa Mkristo hadi kifo; mwendelezo wa mchakato wa elimu kwa vijana na majiundo makini ya Kikristo, ili hatimaye, kuweza kuishuhudia imani kwa njia ya matendo. Waamini watambue kwamba, Injili ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo.

Hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea kuwekeza katika majiundo ya vijana wa kizazi kipya anasema Kardinali Angelo Amato, ili kupambana na utamaduni mamboleo unaosigana na tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili na kijamii; mwelekeo potofu dhidi ya upendo, bidii ya kazi, msamaha na udugu.







All the contents on this site are copyrighted ©.