2013-10-19 11:00:04

Mshikamano wa dhati miongoni mwa wadau mbali mbali ni muhimu katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na utapiamlo wa kutisha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico linasema kwamba, mapambano dhidi ya baa la njaa, utapiamlo wa kutisha na umaskini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, "majanga" haya yanayoendelea kuwadhalilisha mamillioni ya watu duniani yanatokomezwa.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua athari za baa la njaa na umaskini duniani na hivyo kwa pamoja kujitahidi kutafuta mbinu zitakazotokomeza janga hili miongoni mwa watu kwa njia ya maboresho ya mfumo wa chakula. Maaskofu wa Mexico wameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Oktoba.

Kwa pamoja Jumuiya ya Kimataifa ijifunze kujenga na kuimarisha utawala bora, sera makini za uchumi na kijamii ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kuheshimu, kulinda na kutunza mazingira; sanjari na utoaji wa huduma bora za afya na elimu kwa Jamii husika. Mwelekeo huu utasaidia pamoja na mambo mengine kujenga na kuimarisha mshikamano wa kidugu unaowajibisha.

Maaskofu Katoliki Mexico, wanasema haya yote kwa vile wanaguswa na baa la umaskini, njaa na utapiamlo wa kutisha unaojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Yote haya kwa sehemu kubwa ni mambo yanayosababishwa na baadhi ya watu ndani ya Jamii kutaka kujipatia faida kubwa kwa gharama ya maisha ya maskini duniani.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, suala la ardhi linashughulikiwa kwa umakini mkubwa kwani kuna hatari kwamba, baadhi ya makampuni yanaanza kukwapua maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya faida binafsi kwa kisingizio cha kutaka kuwekeza.

Sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo kwa nchi nyingi duniani iwekewe: sheria, sera na mikakati makini inayozingatia mafao ya wengi, vinginevyo baa la njaa na umaskini litaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga. Hata katika maendeleo ya sayansi na teknolojia bado kuna watu zaidi ya millioni 870 wanakabiliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha wakati kuna kikundi cha watu wachache wanaokula na kusaza, kiasi cha kumwaga chakula, hali inayoonesha tabia ya baadhi ya watu kutoguswa na mahangaiko ya jirani zao.

Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi na zaidi katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na maboresho katika mchakato mzima wa uzalishaji, uvunaji, usambaji na ulaji; daima mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Wakulima wadogo wadogo washirikishwe kikamilifu katika mustakabali wa maisha yao kuhusiana na uuzwaji wa maeneo makubwa ya ardhi, kwa kuhakikisha kwamba, haki zao zinatambuliwa na kuheshimiwa.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico linasema, kila mdau anapaswa kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatokomeza baa la umaskini, njaa na utapiamlo wa kutisha. Hata leo hii, Yesu anaendelea kuwachangamotisha wafuasi wake na watu wote wenye mapenzi mema, kuwapatia chakula wenye njaa!







All the contents on this site are copyrighted ©.