2013-10-19 11:44:59

Canada waguswa na mateso na mahangaiko ya wananchi wa Syria!


Shirika la Maendeleo na Amani la Baraza la Maaskofu Katoliki Canada kwa kushirikiana na Serikali ya Canada limechangia zaidi ya dolla millioni 5 kama sehemu ya msaada kwa wananchi wa Syria wanaoendelea kuteseka kutokana na mgogoro wa kivita nchini humo.

Msaada huu unapania pia kuziwezesha nchi kama Uturuki, Lebanon na Yordan ili ziweze kuhimili kishindo cha ongezeko la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Fedha hii ni mchango wa waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wananchi wa Syria. Shirika la Maendeleo na Amani linatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas pamoja na Mashirika ya misaada kimataifa yaliyoko nchini Syria.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu millioni 2 ambao wamekimbilia katika nchi jirani na wengine, millioni 5 wameyakimbia makazi yao. Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Syria na hivyo kusaidia kuchangia kwa hali na mali.

Wito wa Baba Mtakatifu umepokelewa kwa mikono miwili na wananchi wa Canada ambao wanaendelea kuchangia, kielelezo cha imani katika matendo. Kwa njia ya mshikamano wa upendo, Mashirika ya misaada kutoka Canada yataweza kuwahudumia waathirika wa mgogoro wa kivita nchini Syria.







All the contents on this site are copyrighted ©.