Utetezi wa haki msingi za binadamu ni msingi thabiti wa mapambano dhidi ya umaskini
duniani!
Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 17 Oktoba 2013 imeadhimisha Siku ya Kupambana na
baa la umaskini duniani, iliyoongozwa na kauli mbiu "kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa
ubaguzi: kwa kujenga kutokana na uzoefu na ufahamu wa watu wanaoishi katika umaskini
wa kutupwa".
Jumuiya ya Kimataifa imetafakari, lengo la kwanza la Maendeleo
ya Millenia, ifikapo mwaka 2015, ili kuondokana na baa la njaa sanjari na maboresho
ya huduma ya afya. Takwimu za Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF
zinaonesha kwamba, bado kuna idadi kubwa ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano
wanaofariki dunia kila siku kutokana na utapiamlo wa kutisha.
Maadhimisho
ya Siku ya Chakula Duniani na Siku ya Kupambana na Baa la Umaskini Duniani ni changamoto
kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, mambo haya mawili yanapatiwa ufumbuzi
wa kudumu, kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu.
Baa la umaskini duniani linawanyima watu wengi fursa ya kupata rasilimali, kutumia
kikamilifu uwezo wao katika kupambana na hali ya maisha; ukosefu wa usalama na mahitaji
msingi. Matokeo yake ni kushindwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika medani mbali
mbali za maisha.
Jumuiya ya Kimataifa inaalikwa kwa namna ya pekee, kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na kuondokana na falsafa ya ubaguzi
ambayo imekuwa ni chanzo kikubwa cha majanga katika maisha ya Jamii nyingi duniani.
Utetezi wa haki msingi za binadamu ni msingi thabiti wa mapambano dhidi ya baa la
umaskini pamoja na kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya
Jamii.