2013-10-18 08:28:15

Shikamaneni, tafuteni mafao ya wengi, changamoto za sasa ni mapito ya mchakato wa Katiba mpya!


Dr. Adelardus Kilangi, Mwenyekiti wa Tume ya Sheria za Kimataifa, Umoja wa Afrika katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, mchakato wa Katiba ya Tanzania ni fursa ya pekee kwa watanzania katika historia kuweza kushiriki moja kwa moja katika kutunga Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama. Katiba zote zilizotangulia zilitungwa na makundi ya watu kwa niaba ya watanzania wengine. RealAudioMP3

Kwa maoni yake anasema, mchakato wa Katiba unaendelea vyema na kwamba, tayari Rasimu ya Katiba Mpya imekwisha kupatikana na Bunge maalum la Katiba litaundwa hivi karibuni ili kupitisha au kuukataa Mswada wa Katiba Mpya ya Tanzania na hatua itakayofuata ni kurudisha Muswada huo kwa wananchi ili waweze kuupigia kura ya maoni.

Dr. Kilangi anasema, mchakato huu unaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi hasa zaidi ni: kukosekana kwa msimamo wa pamoja kuhusu suala la Muungano, Serikali katika muungano na mawazo baadhi ya watu kwamba, mchakato umetekwa na Chama cha Mapinduzi. Ikumbukwe kwamba, hizi ni changamoto za kawaida katika mchakato wa kutunga Katiba ya Nchi yoyote ile.

Dr. Kilangi anasema, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watanzania wanaendelea kushikamana kwa dhati, daima wakitafuta hatima yao kama watanzania; wadau mbali mbali washiriki katika mchakato kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kikundi fulani cha watu ndani ya Jamii ya Watanzania. Watanzania wakizingatia ushauri huu, watafanikiwa kupata Katiba mpya hata kama kwa sasa inaonekana kwamba, kuna changamoto nyingi!







All the contents on this site are copyrighted ©.