Rais Mahmoud Abbas akutana na kuzungumza na Papa mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 17 Oktoba 2013 amekutana na kufanya mazungumzo
na Bwana Mahmoud Abbas kiongozi wa Wapalestina mjini Vatican. Baba Mtakatifu amewataka
Wapalestina na Waisraeli kufanya maamuzi magumu kwa ajili ya kulinda na kudumisha
amani itakayoungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
Bwana Mahmoud pamoja na
ujumbe wake alikutana na kuzungumza pia na Askofu mkuu Dominique Mambert, Katibu mkuu
wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Katika mazungumzo
kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake, kwa pamoja wamegusia hali ya Mashariki
ya kati na kwa namna ya pekee wamekazia umuhimu wa kuendeleza majadiliano kati ya
Israel na Palestina. Pande hizi mbili zimeonesha matumaini kwamba, suluhu ya amani
inaweza kupatikana na hatimaye, amani ya kudumu kuweza kutawala kati ya mataifa haya
mawili; amani itakayoungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
Kwa pamoja viongozi
hawa wawili wameguswa na hali tete nchini Syria na kwamba, wanatumaini kuona kuwa
wadau wanaohusika na mgogoro wa Syria wataanzisha mchakato wa majadiliano na upatanisho
ili kung'oa mzizi wa vita mapema iwezekanavyo. Wameridhika na uhusiano baina ya pande
hizi mbili na kwamba, wataendelea kufanya upembuzi yakinifu ili kuwa na makubaliano
mapana zaidi katika maisha na utume wa Kanisa huko Palestina.
Baba Mtakatifu
na mgeni wake, wamezungumzia pia kuhusu hali ya Jumuiya za Wakristo katika eneo la
Wapalestina na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Wameguswa na mchango wa hali
na mali unaotolewa na Wakristo kwa ajili ya mafao ya wengi.