Papa kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu wawili, hapo tarehe 24 Oktoba 2013
Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza anatarajiwa kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu
wateule: Monsinyo Jean Marie Speich kutoka Jimbo Katoliki la Strasburg, Ufaransa na
Monsinyo Giampiero Gloder kutoka Jimbo Katoliki Padova, Italia, hapo tarehe 24 Oktoba
2013, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, majira ya jioni.
Itakumbukwa
kwamba, Askofu mkuu mteule Jean Marie Speich alizaliwa kunako tarehe 15 Juni 1955.
Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 9 Oktoba
1982. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Ghana na hapo
hapo kumpandisha cheo na kuwa Askofu mkuu tarehe 17 Agosti 2013.
Askofu mkuu
mteule Giampiero Gloder alizaliwa kunako tarehe 15 Mei 1958. Baada ya masomo na majiundo
yake ya kikasisi, akapadrishwa tarehe 4 Juni 1983. Baba Mtakatifu Francisko alimteua
kuwa Balozi na Rais wa Baraza la Kipapa la Taasisi za Kikanisa, hapo tarehe 21 Septemba
2013.