2013-10-17 15:00:30

Tanzania na China watiliana mkwaju wa mikataba mitano!


Serikali ya Tanzania imeasaini mikataba ya makubaliano (MoUs) mitano ambayo itasadia kutoa fursa za biashara, mafunzo na masuala ya sayansi na teknolojia kwa Watanzania.

Mikataba hiyo imetiwa saini Alhamisi, Oktoba 17, 2013 mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri Mkuu wa China, Mhe. Li Keqiang mara baada ya viongozi hao kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali jijini Beijing, China.

Mikataba hiyo ni Mkataba wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia; Mkataba wa Kuruhusu bidhaa za baharini ziweze kuuzwa China; Mkataba wa Ushirikiano baina ya Tanzania na China kwenye masuala ya Utalii. Mingine ni Mkataba wa Makubaliano baina ya Tanzania na China wa kuanzisha Ukanda wa Kisasa wa viwanda vya nguo pamoja na kukuza zao la pamba na wa mwisho ni mkataba wa kutoa vitalu namba 60 na 61 kwa ajili ya ujenzi wa ubalozi wa China jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya pili ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alimweleza Waziri Mkuu wa China kwamba anaishukuru Seriklai ya nchi hiyo kwa misaada mbalimbali ambayo China imekuwa ikiitoa kwa Tanzania.

“Tunaishukuru kwa misaada mbalimbali na mikopo ambayo imekuwa ikitolewa kwa masharti nafuu ikilinganishwa na mikopo ya kibiashara ambayo hutolewa na nchi nyingine na kawaida ina gharama kubwa kwa Taifa,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake.

Alisema alitumia fursa hiyo kusisitiza uwekezaji kwenye sekta za kilimo, nishati, elimu na miundombinu hasa reli, bandari na teknohama. Kwenye kilimo, Waziri Mkuu alikumbusha suala la upatikanani wa soko kwa zao la tumbaku lakini akaomba uwepo umuhimu wa pekee kwa wawekezaji wa viwanda vya kusindika korosho katika mikoa ya kusini.

“Katika ziara yangu nitapenda kusisitiza haja ya uwekezaji kwenye zao la korosho... nitazungumza na maafisa wanaohusika ili tuone jinsi ya kulipa msukumo zao hili ambalo lina soko kubwa sana hapa China,” alisema.

Alimweleza Waziri Mkuu wa China dhamira ya Serikali ya Tanzania kulipa deni la dola za marekani milioni 24.6 ambalo lilitolowa kama mkopo kwa ajili ya kufufua kiwanda cha nguo cha urafiki.

“Tumeahidi kuanza kulipoa deni hilo katika mwaka wa fedha 2014/2015. Waziri wa Fedha alishaandika barua kwa Serikali ya China tangu mwezi Septemba kuonyesha nia ya Serikali ya kulipa deni hilo,” alisema Waziri Mkuu

Ijumaa, Oktoba 18, 2013 Waziri Mkuu atafungua mafunzo ya siku 10 kwa maafisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali za hapa nchini yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania; atatembelea kiwanda cha Aluminium hapa Beijing, atakutana Bodi ya Tumbaku, Kampuni za Umeme za China Power Investment (CPI) na State Grid Corporation. Pia atakutana na kampuni ya mafuta ya CNOOC. Jioni atakutana na Watanzania waishio Beijing kwenye ubalozi wa Tanznaia nchini China.








All the contents on this site are copyrighted ©.