2013-10-17 15:55:57

Siku ya Chakula Duniani 2013:Papa akemea kashfa ya njaa na utandawazi wa kutojali matokeo yake mabaya.


Katika kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani, Oktoba 16, 2013, Ujumbe wa Papa Francisko umelaumu mwendelezo wa kashfa ya njaa na utapiamlo katika dunia ya leo na kile alichokiita utandawazi wa kutojali kama matokeo yake mabaya.


Hotuba ya Papa Francisko ilitolewa na Monsignor Luigi Travaglino , wakati wa sherehe za Siku ya Chakula Duniani, zilizo fanyika Makao Makuu Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, yaliyoko hapa Roma. Katika ujumbe huo, Papa amekosoa kile alichokiita " kukua kwa mwelekeo wa binadamu kutojali hali za wengine ambako huongoza katika tabia ya kubaguana,iwe kati ya mtu na mtu , kama taasisi au hata katika ngazi ya nchi kwa nchi. Na hasa katika namna za kujali tatizo la uhaba wa chakula, na njaa kali kwa baadhi ya watu , kama vile ni janga lisilo weza kuepukika.


Papa ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, kuvunja ubinafsi na utumwa wa watu wchache kutaka faida kubwa kwa gharama zote, si tu katika mahusiano ya binadamu lakini pia katika mienendo ya kimataifa ya kiuchumi na kifedha. Ili kuishinda njaa , amesema, watu wenyewe wanahitajika kujielimisha upya, juu ya thamani na maana ya mshikamano, neno linaloonekana kukera na kuondolewa katika lugha ya wenye navyo.


Papa amekosoa ubinafsi huo, akitazamisha katika ukweli kwamba, karibia moja ya tatu ya chakula chote kinacho zalishwa duniani huishia katika mapipa ya taka.Na hivyo anasema, kuna haja ya kurekebisha mitindo ya maisha, ikiwa ni pamoja na mazoea ya kula. Uharibifu huu wa chakula , anaoonekana ni matokeo ya utamaduni wa kutupilia mbali, ambao kwa mara nyingi hutokana na roho ya ubinafisi na ubabe wa wanaume na wanawake, kuabudu miungu ya faida na ulaji.


Papa ameutaja udhaifu huo kuwa ni, ishara ya kusikitisha , zinazo onyesha utandawazi wa kutojali wengine ambao, taratibu hutufanya kuyazoea mateso ya wengine na kuona kama ni maisha ya kawaida kwao.

Alihitimisha ujumbe wake kwa wito wa elimu katika mshikamano na maisha kwa ajili ya kupata ushindi dhidi ya utamaduni wa tupatupa au ukimwanga wenye kudharirisha hadhi ya ubinadamu na heshima yake. Ametaka ubinadamu na utu wake uwe kiini cha kuthaminiwa sana katika hatua zote za maisha, ustawi na maendeleo ya kila mtu. .








All the contents on this site are copyrighted ©.