2013-10-17 10:00:34

Rushwa ni janga la mataifa Kusini mwa Afrika!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linasema, rushwa, wizi wa mali ya umma na ufisadi ni vitendo vinavyowaibia wananchi maskini, kiasi hata cha kushindwa kujikwamua katika mchakato wa kujiletea maendeleo endelevu. Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika katika Waraka wake wa kichungaji dhidi ya ufisadi linasema kwamba, hili ni janga la kitaifa, linalopaswa kushughulikiwa kikamilifu.
Fedha iliyoibwa kutoka Serikalini, ingeweza kusaidia mchakato wa maboresho ya makazi ya mamillioni ya watu Kusini mwa Afrika. Ni fedha ambayo ingetoa mchango mkubwa katika kuboresha huduma ya afya kwa mamillioni ya wananchi wanaoendelea kukata tama kutokana na ukata, hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha. Hii ni fedha ambayo kwa hakika ingeweza kusaidia maboresho ya watu wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linasema, rushwa na ufisadi ni hatari kwa Jamii ya watu. Rushwa na ufisadi kwa sasa ni mambo yanayoonekana kuwa kama sehemu ya mtindo wa maisha ya wafanyakazi wengi Serikalini; wafanyabiashara na hata Wakristo ambao wanapaswa kuonesha mfano bora wa maisha adili. Hili ni kundi la watu ambalo limesahau wajibu na dhamana yake kwa Jamii na sasa linajishughulisha na kutafuta fedha kwa gharama ya watu wengine.
Vitendo vya rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanawafanya watu kutoguswa kabisa na mateso wala mahangaiko ya jirani zao. Kwa mantiki hii ya maisha, wananchi wengi wanaondoa imani kwa viongozi waliowachagua na watu wanaowaheshimu kutokana na nyadhifa zao kwa Jamii.
Takwimu zilizokusanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika zinaonesha kwamba, nusu ya wananchi Kusini mwa Afrika, wamekwishawahi kutoa rushwa kwa Jeshi la Polisi au viongozi wa Serikali. Kutokana na ukweli huu, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ni changamoto kwa wananchi wote, kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake katika Jamii. Umefika wakati wanasema Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika kukataa katu katu kutoa au kupokea rushwa kwa kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linadhamiria kuendesha kampeni dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi, Kusini mwa Afrika, kwa kupitia Tume ya Haki na Amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linalojumuisha: Afrika ya Kusini, Swaziland na Bostwana.








All the contents on this site are copyrighted ©.