Makatekista ni majembe katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina!
Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Tafakarini jinsi walivyoishi
na matokeo ya mwenendo wao, mkaige imani yao . Ebr. 13:7. Ni tafakari inayoletwa kwako
na Padre Pambo Mkorwe, OSB, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.
Awali
ya yote, tumwelewe Katekista kama mtu aliyesheheni mafundisho ya Imani [yaani Katekesi],
na hivyo huwajibika katika kuwafundisha watu maundisho hayo, ili watu wapate kuijua
imani yao na kuiishi na pia kuiishi miongozo adilifu tunayopewa na Mama Kanisa Mtakatifu.
Katika mazingira yetu ya kawaida, Katekista huitwa pia mwalimu wa Dini. Mwalimu huyu
wa dini huchukua nafasi yake, mara baada ya ngazi ya familia na huendelea na wajibu
huo hadi mwisho wa maisha yetu ya imani.
Ni yeye huwaandaa watu kwa ajili
ya sakramenti ya Ubatizo, huwatayarisha wazazi wanaomleta mtoto kwa ajili ya ubatizo;
huwatayarisha vijana wetu kwa ajili ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Kipaimara.
Huwaandaa waamini kabla ya kupokea Sakramenti ya ndoa. Na pia katika mazingira yaliyo
mengi, Katekista hushughulika katika kuwazika wafu wetu.
Kwa hayo yote, tunaona
kuwa Katekista/Mwalimu wa dini ni mhimili haswa katika maisha yetu ya Imani. Mwamini
Mlei, amep;itia mikononi mwa Katekista, Makatekista wenyewe wametokana na kazi ya
Makatekista; Watawa nao, wamepitia mikononi mwa Makatekista, Mapadre, ni matunda ya
kazi njema ya makatekista, Maaskofu ni matunda ya kazi ya Makatekista, Makardinali,
Papa na waamini wote wenye wadhifa mbalimbali katika Kanisa na Serikali, sote tu matunda
ya kazi njema ya Katekista, aliyetufundisha imani na maadili. Katika hayo yote, ebu
tuone uzito na umaana wa kazi ya Katekista.
Baada ya kutmbua hayo, tujiulize
sisi sote, ni namna gani tunaenzi kazi ya makatekista, ikiwa ni pamoja na kuchangia
hali njema ya maisha ya makatekista. Waamini wapendwa, hapa tufikiri zaidi juu ya
jukumu letu la kuwategemeza Makatekista wetu, ili waendelee kuitenda kazi yao kwa
ufanisi zaidi. Wito huu utuelekee kwanza kabisa sisi Mapadre, tukitambua kwamba, Makatekista
ndio mikono yetu ya kuume katika utumishi wetu hasa huko maparokiani na vigangoni,
pia katika jumuia ndogondogo.
Pia waamini walei waguswe na mwito huu wa kuwategemeza
Makatekista, kwani katika dunia yetu ya leo, kwa kiasi kikubwa sana, kwani mafundisho
yale ya imani yaliyopaswa kutolewa na wazazi katika familia, wazazi hawafanyi hivyo
kutokana na visingizio mbalimbali na badala yake Makatekista wetu ndio hutusaidia
katika kazi hiyo. Tunawategemezaje? Tufikiri kwa pamoja juu ya uzito na umaana wa
kazi yao , na tusaidie kuinu hali yao ya maisha.
Pamoja na wito huo kwa Mapadre
na Waamini, tumrudie Katekista mwenyewe! Unajionaje katika utume wako? Umeupokea utume
wako kama kazi ya msingi kabisa katika maisha ya Imani ya watu wa Mungu? Katekista,
tambua kwamba wewe ni Mwalimu na Kiongozi wa watu. Hivyo, ili utume wako uwe na maana
haswa ni vema sana ukajijengea haiba ile ya mwalimu mwema na mwadilifu. Ukizingatia
uadilifu basi hata neno utakalolisema litakuwa na mamlaka.
Kwa kuwa Katekista,
hapo tayari una madaraka kama mwalimu. Lakini je, madaraka yako yana mamlaka. KATEKISTA
WEWE NI KIONGOZI, BASI NA UWE KIONGOZI MWENYE MADARAKA NA MAMLAKA. Hapo ndipo unapoalikwa
kwa uweza wako wote kuishi maisha yaliyo adilifu, maisha yaliyo kielelezo bora kwa
wale uwafundishao. Usipokuwa mwadilifu, utakosa mamlaka; yaani mafundisho yako hayatakuwa
na nguvu ya kufundisha, kuonya, kuelekeza wala kusahihisha. Waamini wanapenda pia
kuona unakiishi kile unachokisadiki na kukifundisha.
Jitoe kikamilifu katika
utume wako, ukitanguliza utukufu wa Mungu mbele, nawe utapata yote yaliyo mema sasa
na halafu. Fanya kila uwezazo ili upokeleke na ukubalike na watu kwa maisha yako adilifu.
Ni hapo tu ndipo utaona faraja kuu katika utumishi wako. Basi, na uufanye utumishi
wako uwe furaha yako.
Mungu akubariki na kukutegemeza katika utumishi wako
mwema na mwaminifu, na mwisho wa kazi yako njema sana hapa duniani, wewe pamoja na
wote uliowahudumia, mkastahili kufika mbinguni, Amina.