2013-10-17 08:29:44

Kashfa ya baa la njaa na utapiamlo duniani!


Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaboresha mfumo wa chakula ili kupambana kufa na kupona na baa la njaa na utapiamlo duniani. Hiki ndicho kiini cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo kwa Mwaka 2013 yanaongozwa na kauli mbiu "watu wenye afya wanategemea mfumo bora wa chakula". Maadhimisho haya kwa namna ya pekee yamefanyika kwenye Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO yaliyoko mjini Roma.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho haya uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Luigi Travaglino anasema, ni kashfa kwa dunia kuendelea kuwa na watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa na utapiamlo. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye nchi 150, wanachama wa FAO, kama sehemu ya kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa FAO, hapo tarehe 16 Oktoba 1945. Maadhimisho haya yamefanyika wakati kuna watu millioni 842 wanaobaliwa na baa la njaa na utapiamlo.

Baa la njaa anasema Baba Mtakatifu Francisko ni matokeo ya ubinafsi, falsafa ya kutowajali wengine, kiasi cha kuona kwamba, baa la njaa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Baa la njaa na utapiamlo ni majanga yanayomwandama mwanadamu na wala si sehemu ya mfumo wa maisha yake. Kutokana na changamoto hii kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inafanya mabadiliko sanjari na kuboresha mfumo wa chakula kwa kukazia pia mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu haina budi kujenga utamaduni wa mshikamano pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na matumizi bora ya chakula, kwani kuna kiasi kikubwa cha chakula kinachotupwa kila siku, wakati ambapo kuna watu wanateseka kwa baa la njaa na utapiamlo.

Kwa upande wake Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO, katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani anasema, uhakika wa usalama wa chakula unaweza kufikiwa, ikiwa kama kuna mfumo makini wa chakula unaoweza kuzalisha chakula kinachotosheleza mahitaji ya wengi. Hali ya chakula inaonesha kwamba, kuna watu wachache wanaokula na kusaza wakati ambapo kuna kundi kubwa la watu wanaoogelea katika baa la njaa na utapiamlo.

Gharama za baa la njaa zinatisha kwani, dunia inapoteza kiasi cha asilimia tano ya nguvu ya uzalishaji mali duniani, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la huduma za afya. Dunia inaweza kufaidika kiuchumi, ikiwa kama baa la njaa na utapiamlo litaweza kudhibitiwa kikamilifu. Kati ya nchi 128, ni nchi 62 tu ndizo ambazo zimefanikiwa kufikia lengo la Maendeleo ya Millenia kwa kufuta baa la njaa na utapiamlo, hali inayoonesha kwamba, ushindi dhidi ya baa la njaa ni jambo linalowezekana, ikiwa kila mdau atatekeleza dhamana na wajibu wake.

FAO inasema kwamba, Siku ya Chakula Duniani ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya upembuzi yakinifu ili kubainisha tiba itakayoganga baa la njaa na utapiamlo duniani na kwamba, majanga haya ni matokeo ya mfumo mbovu wa chakula.

Akichangia mada kwenye Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Mama Nadine Heredia, mke wa Rais wa Perù, amewataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa dira na mwongozo utakaosaidia kupambana na baa la njaa na utapiamlo sanjari na kuzingatia: afya, elimu na usawa wa kijinsia, kwa kuwekeza zaidi kwa wanawake kwani hawa ni wadau wakubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo.

Anasema, Jumuiya ya Kimataifa inahitaji sera makini za kiuchumi zitakazosaidia ukuaji wa uchumi na maboresho ya maisha ya kijamii, mambo yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji katika huduma makini za kijamii. Ukuaji wa uchumi hauna budi kuleta faida kwa wananchi wengi zaidi: kwa wale wanaoishi vijijini na mijini; wanawake kwa wanaume.

Wakati huo huo, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inatoa chakula kwa watu wanaokufa kwa njaa pamoja na kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu katika mapambano dhidi ya njaa na utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Naye Kanayo Nwanze, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Kuendeleza kilimo na chakula, IFAD anasema, wakulima wadogo wadogo wanachangia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya mfumo wa chakula, ikiwa kama watabahatika kuwa na miundo mbinu bora, siasa safi, elimu, ujuzi na maarifa. Haya ni mambo ambayo yamejionesha nchini Brazil, Cina, Malasiya na Vietnam, kiasi kwamba baa la njaa kwa sasa limepewa kisogo.

Anasema, IFAD itaendelea kushirikiana na Serikali mbali mbali duniani, ili kuhakikisha kwamba, zinaibua sera na mikakati makini, ili kuwekeza katika miundo kwa nia ya kupambana na baa la njaa duniani.

Wanawake wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo. Ni mchango kutoka kwa Ertharin Cousin, Mkurugenzi mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo wa Umoja wa Mataifa. Anasema, mikakati mingi vijijini, bado inaendelea kuwabagua wanawake, hili ni jambo ambalo halina budi kusitishwa mara moja ili kuleta ufanisi katika maboresho ya mfumo wa chakula duniani. Wanawake wakiwezeshwa, watachangia kwa kiasi kikubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuweza kufikia malengo yake ya kupambana kufa na kupona na baa la njaa na utapiamlo duniani.

Mchakato huu hauna budi kuungwa mkono na mabadiliko ya tamaduni kwa kutambua kwamba, chakula ni haki msingi ya binadamu na kwamba, kila mtu anayo haki ya kuwa na uhakika wa chakula. Jambo hili linawezekana ikiwa kama watu watabadilisha tabia na utamaduni wa kutupa chakula wakati kuna mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na utapiamlo. Ni mchango wa Bwana Nunzia De Girolamo, Waziri wa Sera ya kilimo, chakula na misitu wa Italia, wakati akichangia mada katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2013, mjini Roma.







All the contents on this site are copyrighted ©.