Umuhimu wa sheria za kimataifa katika kuratibu mahusiano mbali mbali Barani Afrika!
Dr. Adelardus Kilangi mwenyekiti wa Tume ya Sheria za Kimataifa kwenye Umoja wa Afrika
katika mahojiano maalum na Radio Vatican abainisha kwamba, Umoja wa Afrika katika
miaka ya hivi karibuni umetambua umuhimu wa kuanzisha tume ya sheria za kimataifa.
Sheria za
kimataifa ni muhimu sana katika kuratibu uhusiano kati ya nchi za Kiafrika na nje
ya Bara la Afrika; mwendelezo wa utengamano kikanda; utekelezaji wa matamaniko makubwa
ya Bara la Afrika na maendeleo endelevu kwa watu wake; ukuzaji na udumishaji wa demokrasia
ya kweli. Haya yote anasema Dr. Kilangi ni mambo ambayo yanapaswa kuratibiwa na sheria
za kimataifa.
Tume ya sheria za kimataifa ya Umoja wa Afrika inaundwa na Makamisheni
kumi na mmoja kutoka katika nchi 54 zinazounda Umoja wa Afrika. Hii ndiyo tume inayojikita
zaidi na zaidi katika utoaji wa ushauri wa sheria za kimataifa kwa nchi wanachama
wa Umoja wa Afrika. Hii ni fahari kwa Tanzania na kwa Chuo Kikuu cha SAUT cha Tanzania
kupata mwakilishi katika tume hii ya kimataifa.