Kila mwaka ifikapo tarehe 16 Oktoba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Chakula
Duniani ambayo kwa Mwaka 2013 inaongozwa na kauli mbiu "watu wenye afya wanategemea
mfumo bora wa chakula".
Hii ni siku ambayo Jumuiya ya Kimataifa inafanya tafakari
ya kina kuhusu umuhimu wa maboresho ya mfumo wa usalama wa chakula na lishe, utunzaji
bora wa chakula pamoja na changamoto kwa wadau mbali mbali kuchangia katika mchakato
wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula
Duniani yatahitimishwa hapo tarehe 20 Oktoba kwa wakazi wa Roma kushiriki katika mbio
za Marathoni, ili kuchangia mfuko wa uhakika wa usalama wa chakula duniani.
Tukio
hili linaadhimishwa kwa namna ya pekee kwenye Makao Makuu ya Shirika la Chakula na
Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO yaliyoko mjini Roma, sanjari na kumbu kumbu ya kuanzishwa
kwa FAO kunako mwaka 1945. Takwimu za FAO zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kwamba,
kuna zaidi ya watu millioni 842 wanaokabiliwa na lishe duni. Jumuiya ya Kimataifa
imeendelea kushuhudia uhalibifu mkubwa wa mazingira unaosababisha athari katika mabadiliko
ya tabianchi. FAO inasema, mambo yote haya yanatishia uhakika wa usalama wa chakula
kwa siku za usoni.
Mfumo wa Chakula unajengeka katika mazingira, watu na taasisi
mbali mbali, mchakato unaowezesha upatikanaji wa mazao ya kilimo, yanayosindikwa na
hatimaye kuwafikia walaji. Kila hatua ya mchakato huu ina athari zake katika maisha
ya mlaji ambaye anapaswa kuchagua lishe bora zaidi.
Maadhimisho ya Siku ya
Chakula Duniani iwe ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya tafakari ya kina kuhusu
mustakabali wa mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani.