2013-10-16 11:29:21

Sala na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Idd El Hajj


Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali Barani Afrika wanawatakia kheri na baraka waamini wa dini ya Kiislam wanapoadhimisha Siku kuu ya Idd El Hajj, siku kuu muhimu sana kwa waamini wa dini ya Kiislam wanapokumbuka utii na unyenyekevu uliooneshwa kwa namna ya pekee na Mzee Ibraham, Baba wa Imani, alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kumtoa sadaka, mwanaye wa pekee!

Lakini inasikitisha kuona kwamba, hata kwa Mwaka huu, Siku kuu ya Idd El Hajj inaadhimishwa wakati ambapo bado kuna vitendo vingi vya umwagaji wa damu kwa watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia. Bado kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini, ujinga, maradhi na njaa pamoja na ukosefu wa mahitaji msingi ya binadamu.

Kilio na mahangaiko ya watu hawa ni chachu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana na kushirikiana kwa pamoja katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli, daima wakiheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini.

Ni ujumbe wa matashi kutoka kwa Baraza la Maaskofu wa Niger kwa waamini wa dini ya Kiislam nchini humo. Siku kuu ya Idd El Hajj ni changamoto muhimu ya kuonesha upendo na mshikamano kati ya watu, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni asili ya uhai unaopaswa kulindwa na kuheshimiwa.

Inasikitisha kuona kwamba, hata leo hii bado damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika huko Mashariki ya Kati kutokana na vita na wakati mwingine baadhi ya watu hufanya vitendo kama hivi wakidhani kwamba, ni kwa ajili ya kumheshimu Mungu, kumbe ni kinyume chake.

Waamini wa dini na madhehebu mbali mbali wanachangamotishwa kushikamana pamoja ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Yote haya yanawezekana ikiwa kama waamini watajikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; sala na matendo ya huruma.







All the contents on this site are copyrighted ©.