2013-10-16 10:31:22

Msumbiji yaukumbuka wema na ukarimu wa Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere!


Wananchi wa Msumbiji na Wanatanzania wanaoishi nchini Msumbiji kwa pamoja, jumapili iliyopita waliungana katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 14 tangu alipofariki dunia mtumishi wa Mungu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri unaendelea Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu mwenye imani kuu na mwanasiasa mahiri na kila jambo alilipatia nafasi yake na kamwe hakuchanganya mambo. Ni kiongozi aliyepigania haki msingi za binadamu, akakazia uhuru, umoja, upendo na mshikamano kati ya watu. Alikuwa ni mtu wa shukrani aliyetambua nafasi ya Mungu katika maisha yake kama mwamini na mwanasiasa. Daima alimtanguliza Mwenyezi Mungu katika mipango na mikakati yake ya maisha. Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Padre Joseph Juma, OFM wakati wa kumbu kumbu ya miaka 14 tangu alipofariki dunia Mwalim Nyerere.

Mwalimu anakumbukwa na wengi kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, demokrasia na uhuru wa kweli. Ni kiongozi aliyekuwa na upeo mkubwa katika maisha. Ataendelea kukumbukwa na wengi, wakati huu watu wanapoanza kukengeuka kutokana na udini, ukabila, rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Katika tukio hili ambalo limewagusa wananchi wengi wa Msumbiji wanaokumbuka fadhila na ukarimu wa Mwalimu Nyerere kwa watu waliokuwa wanateseka kutokana na ukoloni. Rais mstaafu Joaquim Chisano wa Msumbiji, amemshukuru Mwalimu kwa mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini mchango wa wapigania ukombozi nchini Msumbiji, akajitosa kimasomaso kuwasaidia kwa hali na mali.

Wakati wa mapambano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji, wananchi wengi waliogopa kwenda kusali Makanisani au misikitini, lakini Mwalimu Nyerere kila wakati alipokuwa anafika nchini Msumbiji, hakukosa kwenda kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Mtakatifu Antonio da Polana.

Ni mwamini na kiongozi aliyeonesha unyenyekevu wa hali ya juu, akawapenda na kupendwa na watu kutoka ndani na nje ya Tanzania. Kwa hakika Mwalimu alikuwa ni mtu wa watu na kamwe hakupenda makuu, kwani kwa wanyonge alikuwa mnyonge ili aweze kuwaonjesha upendo wa kibaba.

Rais mstaafu Chisano anasema kwamba, Mwalimu alipong'atuka kutoka madarakani na baadaye kupata nafasi ya kutembelea tena Msumbiji, Rais Chisano wakati huo, aliamua kumtembeza Mwalimu mjini Msumbiji, ili aweze kujionea hali halisi ya maisha ya watu wa Msumbiji. Alimshauri kuwekeza kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wanauza bidhaa barabarani, ili hatimaye, waweze pia kuchangia katika kuinua uchumi na pato la taifa badala ya kujenga tabia ya kuwa omba omba na wategemezi.

Rais mstaafu Chisano anasema, maneno haya kutoka kwa Mwalimu yameendelea kuwa ni changamoto kubwa katika maisha yake kama Rais na raia wa Msumbiji. Anasema, ili taifa liweze kusonga mbele linahitaji: watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, tunu msingi ambazo zilisimamiwa kwa dhati na Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake, changamoto hata kwa viongozi wengine Barani Afrika.

Naye Dr. Shamin Nyanduga, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji anasema kwamba, Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwaminifu kwa Serikali na dini yake ndiyo maana Jimbo Katoliki la Musoma limeanzisha mchakato wa kutaka atangazwe kuwa Mwenyeheri na hatimaye mtakatifu, kama mfano wa kuigwa na waamini walei.

Ni kiongozi aliyejitahidi kutumia vipaji na karama zake kwa ajili ya mafao ya wengi. Alihamasisha matumizi sahihi ya rasilimali ya taifa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote. Ni kiongozi aliyetegemewa na wengi kwa ushauri kutokana na hekima na busara ambayo alikirimiwa na Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.