Uhusiano na Rwanda, majambazi na wahamiaji haramu, ziara zake nchi za nje, tuzo ya
hifadhi, Baraza la Umoja wa Mataifa, mchakato wa katiba ni kati ya mambo ambayo yameguswa
kwenye hotuba ya Rasi Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania katika hotuba , mwishoni mwa
Mwezi Septemba, 2013.
Ndugu Wananchi; Namshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba salama
na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi kuzungumza nanyi
siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013.
Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya
kupata taarifa ya yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi
ya mambo huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa kuyapuuza,
bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali pengine pa kuyasemea.
Uhusiano
na Rwanda Ndugu Wananchi; Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi
wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri na tatizo la
ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita na Kagera. Nafurahi kusema
kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia moyo.
Tarehe 5 Septemba,
2013, nilikutana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala.
Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu kuzungumzia
uhusiano baina yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa mazuri na sote tulikubaliana
kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze
mazingira yatakayosaidia kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema
kama ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi wa umma,
wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa ujumla tusaidie kuimarisha
uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji
Haramu
Ndugu Wananchi; Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa tutachukua
hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini bila ya kuzingatia taratibu
zinazohusika. Niliwataka majambazi wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale
wanaoishi nchini bila ya kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao.
Nilitoa siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya hapo tungeanzisha
operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo. Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume
cha sheria watu wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng’ombe
8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni kuanza tarehe
6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013, wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa
makwao na watuhumiwa 279 wa unyang’anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu
10 ya kutupa kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo
2 ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng’ombe 8,226 walikamatwa wakichungwa
katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu, mbao 2,105 zilikamatwa pamoja
na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi; Agizo la kuwataka
watu wanaoishi nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au
wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania. Walikuwa
wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo si ya kweli hata kidogo.
Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi 68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya
Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni
kwamba hakuna mtu ye yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka
wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza kulalamika
wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Bahati nzuri jambo
hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi; Yalikuwepo pia madai kwamba
tunawaonea na kuwatesa watu walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo waambiwe
kuwa siyo raia. Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia haupatikani kwa kuishi nchi
ya kigeni kwa miaka mingi. Unapatikana kwa kutimiza masharti ya kuomba na kupewa
uraia. Kama mtu hakufanya hivyo anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka
wazazi wake. Ipo mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia nyadhifa zao
baada ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya Katiba
na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi; Katika kutekeleza operesheni
hii niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa nchini miaka mingi ambao wana nyumba,
mashamba au mali mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana watoto au hata wajukuu waelekezwe
kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao.
Pia niliagiza watu wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika
kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti, taarifa itolewe
kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili hatua zipasazo zichukuliwe.
Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii
kumpongeza Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo
ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika zoezi hili. Pia,
nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji,
Idara ya Mifugo, Idara ya Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali
kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20 Septemba,
2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa endelevu, muda si mrefu
awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu
ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi; Kati
ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013 nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada
na Marekani. Nchini Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa
Shahada ya Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea maendeleo
na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya changamoto zinazotukabili.
Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa
karibu na Wizara zinazohusika na Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine, Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara
hizo na viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu
Wananchi; Nchini Marekani nilikutana na kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali
wa Serikali ya nchi hiyo wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge
la Marekani. Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu
na mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza na kukubaliana
na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni
mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa
na utekelezaji umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa
sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi; Jambo lingine kubwa na
la faraja kwetu ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini
za kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za Milenia
yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa na Bodi ya MCC na
kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani kwa ajili hiyo.
Tuzo
ya Uhifadhi
Jambo lingine muhimu katika safari yangu ya Marekani ni kutunukiwa
tuzo na “International Congressional Conservation Foundation” kwa kutambua juhudi
zetu katika kuhifadhi wanyama pori na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto
mbalimbali tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika jitihada
tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya uhifadhi wa wanyama
na misitu.
Ndugu Wananchi; Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za utayari
wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa kupewa tuzo na katika mkutano
wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika mkutano maalum wa kupambana na ujangili
na biashara ya meno ya tembo duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu
Wananchi; Shabaha kuu ya safari yangu ya Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa
68 wa Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu
ya mkutano wa mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani:
Post 2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama mtakavyokumbuka Malengo ya
Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000, yanafikia ukomo
wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka
huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata hivyo, mjadala huo unaanza
kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000
umefikia wapi mpaka sasa na utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia kwa
ujumla. Tathmini ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza
malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake umefikia shabaha
hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile
vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi; Kwa upande wetu,
Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo: Lengo la Milenia namba
2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2)
Lengo la Milenia namba 3 hasa kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari.
Ukweli ni kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia shabaha
kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu kulifikia ifikapo
2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa Wabunge wanawake na wanaume.
Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo
katika uchaguzi wa 2015 iwapo tutaamua iwe hivyo;
(3) Lengo la
Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri
chini ya miaka mitano; (4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba
6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na (5) Kwa upande wa lengo
namba 7 kuhusu mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini.
Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo ifikapo mwaka 2015
kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika bajeti ya mwaka huu. Lakini,
hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo
mwaka 2015. Safari bado ndefu sana.
Ndugu Wananchi; Malengo ya Milenia
namba 1 na namba 5 ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo
2015. Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza umaskini na
njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua tunazochukua kuleta mageuzi
katika kilimo zina lengo la kuhakikisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima.
Mafanikio yanaanza kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo
mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya Conditional Cash Transfer
ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango
huu utatusogeza sana mbele lakini bado tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza
umaskini ifikapo 2015.
Ndugu Wananchi; Kwa upande wa Lengo la Milenia namba
5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza vifo vya kina
mama wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito wanaojifungua chini ya uangalizi wa
wataalamu wa afya. Hatutaweza kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo
ya Afya ya Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza
ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha upatikanaji wa dawa na
tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha
hatua tuliyopiga mpaka sasa. Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele
zaidi ingawaje bado tutakuwa chini ya lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo
litakuwa historia.
Ndugu Wananchi; Lengo la Milenia namba 8 linazihusu nchi
tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza Malengo ya Milenia.
Bahati mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata
vile wanavyoahidi wenyewe kutoa katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi
zao, sura ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu
Wananchi; Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna
nchi ye yote duniani iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu.
Ushauri wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize ahadi
zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Ilionekana suala la upatikanaji
wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo
ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia
malengo ya 2015 na hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi
ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi; Wakati nikiwa safarini,
tarehe 21 Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la Biashara
la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na zaidi ya 200 walijeruhiwa.
Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi
wa Kenya na kuwahakikishia kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu
kuwa baada ya tukio hilo watu wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama
wetu. Ni hofu ya msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini
ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza maisha.
Ndugu
Wananchi; Napenda kuwafahamisha kuwa tangu shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa
inajenga uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja
mbalimbali. Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na
Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili hiyo. Juhudi
zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya,
vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na
kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza kutokea nchini.
Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri yameshambuliwa. Kilicho muhimu
ni kuendelea kuchukua tahadhari na wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe
zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote wenye shughuli zinazokusanya
watu wengi kama vile maduka, maofisi, mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi
nje na ndani ya maeneo yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal
detectors and x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au gharama, lakini
gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko ya usumbufu huo.
Ndugu
Wananchi; Nawaomba muendelee kufanya shughuli zenu bila ya hofu ingawaje msiache
kuwa makini na kuchukua tahadhari. Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona
mtu au watu au kitu cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii
na taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea kuelimisha umma
kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi Serikalini tumejipanga kuchukua
hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu na watu wake.
Mchakato
wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi; Kama mtakavyokumbuka, Bunge
lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka mchakato
mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei, 2012, Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo
ni kupokea maoni ya wananchi, kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea
maoni ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo
ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya tafakuri
zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi
kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa
tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi; Baada ya Bunge la Novemba, 2011 kupitisha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka sheria hiyo iboreshwe
kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya upinzani na Chama tawala. Majadiliano
yalifanyika baina ya Serikali na vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia.
Makubaliano yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza ihusishe
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho yanayohusu Bunge Maalum
na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko yaliyohusu Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika
mazungumzo kati yao na Serikali na maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho.
Serikali ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi; Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ilitoa mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi wa wajumbe
wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana
na kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa
kufikia maamuzi ndani ya siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia
siku 90. Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika
wa Bunge ambaye nae aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala.
Kama ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao kuhusu Muswada.
Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo mazuri yalitolewa na wadau.
Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge
ambao si Wajumbe wa Kamati walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia
kwamba mjadala ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe
kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi; Nimefahamishwa
kuwa Wabunge wa vyama vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa
ugumu mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata ufumbuzi.
Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali walikubaliana kwa maeneo
mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge
nao wayajadili na kuyapatia ufumbuzi.
Ndugu Wananchi; Baada
ya Kamati kumaliza kazi yake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe
aliwasilisha Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba
ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kutoa maoni
ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Tundu Lissu alitoa maoni
yake.
Ndugu Zangu; Baada ya watu hao watatu kutoa maoni yao ilitarajiwa
kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo hayakuwa hivyo. Badala yake
kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada
usijadiliwe. Ilifikia wakati hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa.
Katika hali isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa
wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya kutetea hoja
zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Pia wamejinyima nafasi
ya kusema mambo mengine wakati wa mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge
waliokuwepo waliendelea kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha.
Walifanya hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi
ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni mwa yaliyokubaliwa
na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum
na lile la ukomo wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi; Kwa
maoni yangu madai ya Kambi ya Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika
kama Wabunge wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na kupitisha
Miswada Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na mtu wa kusema mawazo
yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo
lisilowezekana. Haya ni masuala yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni
na si vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria kama
Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka, hakutaleta mabadiliko
wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao wanautambua ukweli huo.
Ndugu
Wananchi; Kuna msemo wa wahenga kuwa “historia hujirudia”. Naomba hekima ziwaongoze
viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia
mwaka 2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na kuzungumzia
hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na kifanyike vipi. Baada
ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu
Wananchi; Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza
taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo
kila sababu ya kuhoji dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya
kuuliza nia ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na
kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka
kupata Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa ndugu
zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango ya maandamano na
kufanya ghasia. Badala yake watumie njia halali zinazotambulika kikatiba na kisheria
kujenga hoja za kufanya marekebisho wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya kubomoa.
Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari. Ndugu Wananchi; Napenda
pia kuzisemea baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema
kuwa nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa Tume ya
Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu,
Watanzania Wenzangu; Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu Lissu ni uzushi na
uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo
kwa sababu, sipendi kuamini kuwa Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli
au kwa bahati mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine
isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu
na maslahi ya taifa nikiagizwa na Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu
nafahamu ni kazi ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi
hata kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile ya Tume ilikuwa ngumu
kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na waombaji walikuwa wengi mno
kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na 15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi
ya 60 na waombaji walikuwa zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170
zikiwa na waombaji zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si
mtihani mdogo. Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya taifa, yaani
watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini, wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi,
wasomi, Wabunge, Wawakilishi, wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia
n.k.
Ndugu Wananchi; Pamoja na changamoto hizo, lakini tulifanikiwa kuunda
Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu wengi hata wale ambao hawakuteuliwa
wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje? Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi
wa vyama vya siasa vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata
wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA. Ndiyo maana
nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa
ni uongo wa mchana usiokuwa na kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia
waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu ambao wanawakilisha
kundi zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa si kila
taasisi iliyoomba itapata mwakilishi kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo.
Kwa kutumia utaratibu huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa
na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na makundi ya maslahi
mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa kuwateua Wajumbe wa Bunge
Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo
na nafasi za kutosha kila kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum
lisilokuwa na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi; Mimi na Rais wa Zanzibar
tumekuwa tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa na
wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika sasa hata tuonekane
hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema
hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia
akilini. Wakati mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa
zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama hiyo ndiyo
shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu; Hatutengenezi
Katiba ya Chama fulani bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa
na vyama ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe na
msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote wanaostahili au kuwa
na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa Wajumbe, hivyo wale wachache watakao
bahatika lazima wawasemee wote. Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote
hata wale wasiokuwa wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi; Bahati
nzuri hii ndiyo sifa kubwa iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi
ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu
Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea haki. Tunataka watakaokuwa
Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa
letu na watu wake badala ya kujali yale ya taasisi zao au makundi yao.
Zanzibar
Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi; Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya Zanzibar
kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa katika Muswada. Hivyo basi napata
tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi
wake nini! Labda kuna kitu sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati
kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar. Nimeambiwa kuwa
Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati haistahili kulaumiwa. Kama hivyo,
nashauri kuwa suala hili lirudishwe Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia
uamuzi muafaka. Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi,
kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao vya Bunge au
kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi; Nimeambiwa pia
kuwa kulikuwa na hoja ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
iwe sawa kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya Wajumbe
wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi. Ni kwa maelewano
ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo maana idadi imewekwa sawa ili
sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa
theluthi mbili ya kura za kila upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza
kupata bali ni ulinganifu sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi
unaotumika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la
kulinda maslahi ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na Tanzania Bara
ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati Wazanzibari watashindwa. Lakini,
hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara
au kupunguza majimbo ya Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja.
Msingi
unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano wakati wa kuamua
masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako sawa. Hakuna mdogo kumezwa
na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna
kitakachoharibika kwa idadi ya Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo.
Lakini kama Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya
mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi; Katika
orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka
usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka
mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani
na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala.
Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa
mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa
mshirika katika hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa
na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.
Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.
Ndugu
Wananchi; Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi
kuongozwa na hekima iliyotumika wakati tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati
ule inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka salama salimini
bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani. Kupanga ni kuchagua, naomba sote,
mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia
nchi yetu amani, usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.