Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, amewataka watoto kutambua kwamba
wao ni zawadi kutoka kwa Mungu, kwa hiyo jukumu lao kubwa ni kuwa Wamisionari kwa
kuitangaza Injili kila mahali ili wasiomjua Mungu waweze kumkiri na hatimaye, waweze
kuokoka.
Askofu Nyaisonga amesema hayo Jimboni Dodoma katika kituo cha hija
Mbwanga wakati wa adhimisho la Ibada ya misa takatifu ya kongamano la maadhimisho
ya hija ya Mwaka wa Imani kwa watoto wa Shirika la kipapa Jimboni Dodoma. Askofu Nyaisonga
amesema kuwa watoto, wanatakiwa kulisaidia Kanisa kwa kulitangaza Neno la Mungu, kuanzia
majumbani mwao, shuleni, kwenye michezo na kuwahamasisha wengine wampende Mungu na
kuchukia dhambi.
Askofu Nyaisonga pia amewataka watoto wa Tanzania wamuombee
Baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye anatimiza miaka 14 tangu
alipofariki dunia. Amesema ni jukumu la watoto kumuombea ili siku moja Kanisa limtangaze
kuwa mwenyeheri.
Kwa Upande wake Askofu Mstaafu Mathias Isuja Joseph wa Jimbo
Katoliki Dodoma, amewataka watoto kusoma kwa bidii ,ili kwa siku za baadaye waweze
kuishi maisha mazuri.
Na wakati huo huo, Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo
Katoliki Dodoma amewataka Wakristo nchini Tanzania kuishi maisha ya utumwa na kutambua
kuwa Yesu Kristo ndiye mmiliki wao. Amesema kuwa si jambo la aibu kujiita mtumwa bali
ni heshima hasa kuwa mtumwa wa Yesu Kristo kwani Yesu mwenyewe ndiye anaye wajibika
kwa watumwa wake.
Askofu Nyaisonga amesema kuwa wapo baadhi ya watu ambao hawaamini
kama Mungu yupo na kuendelea kutenda Dhambi kwa kuwa hawaoni wala kusikia sauti ya
Mungu ikiwakemea waache uovu wao. Hata hivyo amesema ni vema Wakristo kuwa kama Mtume
Paulo alipo ulilizwa wewe ni nani, naye akajibu mimi ndiye mtumwa wa Yesu Kristo akimaanisha
kuwa yeye ni mali ya Yesu Kwani bila Yesu hawezi chochote.