Kutokana na ongezeko la vitisho na vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia,
Malkia wa Uingereza hivi karibuni alianzisha Wakala wa Kitaifa kwa ajili ya kupambana
na Uhalifu, unaojulikana kama NCA, National Crime Agency. Wakala huu umepewa dhamana
na jukumu la kudhibiti vitendo vya uhalifu nchini Uingereza pamoja na kuendelea kushirikiana
na nchi 150 duniani. Wakala huu utakuwa pia na jukumu la kuangalia mwenendo wa Jeshi
la Polis inchini Uingereza.
Wizara ya Mambo ya ndani ya Uingereza imebainisha
kwamba, wakala huu utaungana pia na taasisi nyingine zilizopo nchini Uingereza katika
kupambana na uhalifu wa kitaifa na kimataifa. Uhalifu kwa njia ya mitandao ya kijamii
ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele kwa sasa sanjari na kulinda mipaka ya nchi
pamoja na watoto. Kikosi cha Scotland Yard, maarufu katika masuala ya upelelezi nchini
Uingereza kitaendelea kujikita katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kitaifa na kimataifa.