Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Tupo pamoja tena katika kumegeana mkate kama lilivyo agizo la Bwana, tayari safari
yetu katika mwaka huu wa Kanisa iko katika kituo cha Dominika ya 27. Bwana azidi kutufundisha
kwa njia ya Neno lake aksema, imani ndogo iliyokamilifu yatenda mambo ya ajabu tusiyoweza
kuyafikiria, ndiyo kusema lazima iwe imani inayokabidhi maisha ya mtu mwenyewe mwenye
imani katika mikono na uweza wa Mungu.
Katika somo la kwanza tunaona Nabii
Habakuki analalamika na kunungunika mbele ya Mungu akisema mbona hataki kusikiliza
kilio chake! Hata hivyo yafaa kutambua kuwa mateso wanayoyapata hawa wana wa Israeli
ni kwa sababu ya ukaidi wao ambao ndio uliowafanya watekwe na makabila mengine. Inavyoonekana
ni mpango wa Mungu kuwaaacha ili waonje nini maana ya kumwacha yeye na kuwaelekea
miungi wengine!
Lakini hata hivyo anawahaidi kama watamgeukia yeye na kujenga
uaminifu tena atawaondoa katika taabu yao hiyo. Mwaliko kwetu ni kujenga imani na
mapendo kwa Mungu kama tunataka kuondokana na utumwa unaosababishwa na ukaidi wa mioyo
yetu na hivi kutupelekea katika anguko la dhambi.
Ndiyo kusema wimbo wa katikati
wa Dominika hii umewekwa mahali pake ukituambia, Ingekuwa heri leo tusikie sauti yake,
tusifanye migumu mioyo yetu. Katika mwendelezo huo Mt Paulo anakuja na agizo kwa Mt.
Timotheo, akimwambia yafaa kuchochea karama uliyopewa kwa njia ya kuwekewa mikono,
na kwa namna hiyo unadaiwa kumshuhudia Kristu kwa nguvu zako zote na hata ikikulazimu
kupata mateso mengi.
Mpendwa msikilizaji, umepokea karama za Bwana kwa njia
ya ubatizo na kwa njia ya sakramenti nyingine basi inakulazimu kuchochea karama hizo
na kuziishi kwa furaha ukimweka Bwana katika nafasi ya kwanza katika maisha yako ya
umisionari. Hapa ndipo kuna kuishi imani yako inayotakiwa ijidhirishe katika kujikabidhi
mikononi mwa Mungu.
Mwinjili Luka anaweka maneno ya Bwana mbele yetu anayetualika
kukua katika imani, ambayo kwayo twaweza kutenda miujiza mbalimbali na hasa mwujiza
mkuu wa upendo. Wajibu wa Mkristu ni kushika imani na kuishi imani hiyo kwa unyenyekevu,
pasipo madai yoyote mbele ya Mungu au mbele ya watu. Jukumu kubwa hilo linatekelezwa
na kuonekana katika Injili Bwana anaposema inatosha tu kusema sisi ni watumwa tusio
na faida.
Ndiyo kusema, Bwana anataka kutuambia tuishi tumaini la kweli katika
Bwana tukitarajia ya kwamba yote atatenda kwa mapendo yake mara baada ya sisi kutekeleza
wajibu wa kuishi imani yetu katika yeye kama Mt Paulo atuambiavyo akisema, kwangu
kuishi Kristo.
Baada ya kuupata huo utangulizi sasa, polepole tujiulize hili
fundisho la Bwana juu ya imani linatoka wapi? Kwa hakika fundisho hili linakuja baada
ya Mitume kumwambia Bwana tuongezee imani, kama ambavyo hata sisi tunalo hitaji la
kujitafiti na kumwomba Bwana tukisema, tuongezee imani! Tukishaweka swali hili mbele
ya Bwana yafaa tena kujiuliza lakini imani ni nini?
Je, ni ujuzi?, Je, ni
maarifa? Je, ni maisha ya utekelezaji wa sheria za kidini au tuseme ni nini? Katika
haya tuliyoyataja kama imani ingekuwa ndo hayo basi imani ingekuwa ni kitu cha kumiliki
na kwa namna hiyo kingekuwa kitu cha kukuzwa!
Kutokana na swali hilo Bwana
anakuja na namna tofauti ya kuitazama imani na anatufundisha nasi kufuata mkondo huo.
Bwana anasema kama mngelikuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu
huu ngoka na ungewatii! Bwana anataka kusema imani haiko katika vipimo vya kimahesabu,
na wala si ujazo bali ni kuitika mwaliko wa Bwana na kujikabidhi nikiwa nilivyo hata
katika udhaifu wangu katika mikono ya Mwenyezi Mungu ambamo hakuna kisichowezekana.
Imani
ni laini mno kama mbegu ya haradali na ni nguvu kwa wakati huohuo iliyo ndani ya mbegu
hiyo ambayo huvunja suke ili maisha yaweze kutokea au kuzaliwa! Imani ni nguvu ya
Kimungu inayoongoza maisha ya mwanadamu anayekubali mapenzi ya Mungu. Kumbe yatosha
kusadiki na kujikabidhi katika nguvu hiyo takatifu.
Kwa imani ndogo yatosha
kubadili maisha yetu kwa maana udogo huu unajikita katika mtima wa Mungu mwenyewe
na kwa namna hiyo hubadili maisha ya ulimwengu, cha msingi ni kuishi imani hiyo kwa
unyenyekevu. Inatosha imani kidogo kuweza kuondoa woga ambao hujitokeza katika maisha
yetu unaotokana na mwenendo na mporomoko wa waamini wakristu katika Kanisa la leo.
Woga huu haupaswi kukua kwa maana kama tukiamini Kanisa huongozwa na Roho Mtakatifu
basi yeye atafanya kazi yake apendavyo na kuliongoza lifikie mwisho wa nyakati.
Kwa
kumtanguliza Roho Mtakatifu tayari tunaingia katika kuepuka kujitafutia utukufu wetu
wenyewe bali utukufu wa Bwana mwenyewe. Ndiyo kusema baada ya kuishi imani yetu, baada
ya kutumikia tunapaswa kusema sisi ni watumwa wasio na faida. Kanisa linapaswa kutumikia
Bwana aliye kichwa chake na wala si mtu mwingine awaye yote likisema mimi ni mtumishi
wa Bwana nitendewe kama Bwana utakavyo. Ni kwa namna hiyo linajikabidhi katika maongozi
ya Roho Mtakatifu mwanzilishi na kiongozi wa Kanisa.
Mpendwa msikilizaji, huu,
ndio wito wako daima kujikabidhi mikononi mwa Mungu ambaye ni chanzo cha maisha yetu
na ukomo wake. Kuishi maisha ya pamoja yanayoongozwa na unyenyekevu unaojikita katika
kuutangaza ukuu wa Mungu anayeongoza Kanisa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nikutakie
heri na furaha daima katika maisha yako yak ila siku ukijitahidi kushiriki zawadi
za Kimungu zitujiazo kwa njia ya imani. Tumsifu Yesu Kristo na Maria.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C,PP.S.