Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 26 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Tunaendelea kama kawaida katika kipindi chetu tafakari masomo Dominika, tayari tumekwisha
safiri hadi Dominika ya 26 ya mwaka C. Katika Injili ya tunayoitafakari Mwinjili Luka
anatupa mfano ambao tunawakuta watu wawili ambao ni Lazaro na yule tajiri mwenye kutumia
hasa mali yake, katika maisha yao hapa duniani na baada ya maisha ya duniani kila
mmoja yuko katika sehemu aliyoitayarisha. Hukumu ambayo inasimuliwa pale iko wazi
na inagota pasipo kupinda katika mahali pake.
Mpendwa msikilizaji tuanze kumtazama
huyu tajiri. Huyu alikuwa tajiri kwa maana halisi ya utajiri, yaani utajiri unaoonekana
wazi. Katika Agano la Kale aliyekuwa tajiri kwa hakika alionekana kubarikiwa na Mungu.
Si tu katika Agano hilo tu bali kwa wakati fulani katika ulimwengu wa kikalvinisti
utajiri ulionekana kama baraka toka kwa Mungu.
Pamoja na hayo mawazo yaliyokuwepo
Bwana wetu Yesu Kristo anakuja na hukumu na fundisho tofauti juu ya utajiri na mali
kwa ujumla. Ukitazama vema huo mfano utaona kuwa huyu tajiri jambo la msingi kwake
ilikuwa ni anasa, kumbe, ni kinyume na baraka toka kwa Mungu, ni kinyume na maadili
na mwenendo mzima wa jamii. Inaonekana pia tajiri huyu hana hata jina wala familia
ndiyo kusema hata utu ni walakini! Ni kwa namna hiyo ile hali ya kuwa katika moto
ilikwishaanza hapahapa duniani! Ni hali ambayo alilipandikiza mwenyewe katika maisha
yake hapa duniani.
Mpendwa mwana wa Mungu, mara moja tunaweza kujiuliza nani
anaingia motoni? Kwa hakika kulingana na mfano huu ni yule ambaye amejifungia katika
ulimwengu wake wa mali na anasa, mchoyo ambaye kwa hakika kumsaidia mtu kama Lazaro
ni kero kubwa. Ni yule ambaye anao woga siku zote wa kupoteza mali yake na hivi hujikomaza
katika uchoyo na kutafuta namna ya kulinda mali yake.
Ni yule ambaye upendo
kwa wengine unaosimikwa katika moto wa mapendo ya Mungu kwa mwanadamu ni sumu au umejengeka
katika mfumo wa mahesabu kama wale ndugu wa wili Kuhani na Mlawi waliompita mteswa
na baadaye mteswa huyo akaja kusaidiwa na Msamaria mwema. Basi mpendwa mwana wa Mungu
angalieni vema namna ambayo ni njema katika kuendesha utajiri ulionao, yaani akili,
mali muda, familia nk ili ukufae kwa maisha ya uzima wa milele.
Mpendwa msikilizaji
yafaa sasa tumtazame huyu Lazaro maskini wa Mungu. Kwa hali yake kimwili katika mazingira
yale isingetarajiwa Bwana kumtazama. Kuna mawazo tangu wakati ule na hata hivi leo
kwamba pengine hali ya umaskini inasababishwa na maskini wenyewe! Inawezekana, lakini
tuangalie mfumo jamii! Pamoja na mawazo hayo Bwana analofundisho tofauti, kwake yeye
maskini ni watoto wa Mungu, na amekuja kwa ajili yao, kumbuka nimepakwa mafuta ili
niwahubirie maskini habari njema, Lk 4:18.
Basi mpendwa, Lazaro anatofautiana
na tajiri kwanza ana jina tofauti na tajiri ambaye hana jina. Jina lake lamaanisha
“Mungu ni Msaada, Mungu nisaidie”. Jambo jingine la kutazama ni kwamba Lazaro yuko
kifuani mwa Ibrahimu akifurahia utukufu wa Mungu. Maana yake nini kuwa kifuani? Ni
kuwa katika kitovu na kisima cha mapendo. Katika msingi huohuo wa kumweka Lazaro katika
mtima wa mapendo, Bwana huwajali wale wote wanaoteseka katika ulimwengu wa leo.
Mpendwa
mwana wa Mungu nini maana ya fundisho hili? Bwana ataka kuwakemea tu matajiri au ataka
nini! Bwana hayuko katika mlengo wa ugomvi na matajiri bali anaonesha kuwa hali ya
namna hii katika jamii ya watu haifai kuendelea yafaa kuiacha na kuishi maisha ya
kugawana sawa kile ambacho Mungu amtujalia sisi sote. Anataka kuonesha kuwa hali ya
kujijenga katika uchoyo yaleta hatari ya kukosa zawadi za Kimungu.
Bwana anakuja
na dunia mbili zilizotengana kwa mtalo mkubwa na yanajitokeza mawazo ya kutuma mmoja
toka ulimwengu wa Lazaro ili akawape habari walioko duniani wakatubu! Jibu kuhusu
mawazo hayo ni kwamba wanao Musa na manabii, wanayo sheria wakafuate hayo na watafika
katika furaha kamilifu.
Mpendwa, hawa ambao wanao manabii na sheria ni akina
nani? Ndio sisi katika ulimwengu wa leo. Tunaalikwa na tunapaswa kushika vema mausia
ya Bwana. Tunaalikwa kugawana sawa mapato yetu, kuishi maisha ambayo yatupa jina tofauti
na tajiri ambaye hana asilia, hana jina, hana familia! Tuwatazame wale ambao wanatamani
kushibishwa kwa makombo na mabaki, ambao wanaishi katika mitaa ambayo haiendani na
hadhi ya mwanadamu aliye kiumbe cha Mungu.
Ninakutakia furaha na amani itokayo
katika maisha ya ushirika mtakatifu katika kujenga familia ya Mungu. Tumsifu Yesu
Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.