Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Nakuleteeni Tafakari masomo ya Dominika ya 24 ya mwaka C wa Kanisa. Injili inatupa
changamoto ni namna gani twaweza kuwa wema katika maisha yetu ya Kikristu. Bwana wetu
Yesu Kristu anapofundisha hupenda kufundisha akitumia mazingira halisi toka mawazo
na kuingia jambo gusika, kumbe, hutumia mifano akitaka kutuambia Mungu Baba ni nani!
Kwa kutumia lugha halisi na mifano Bwana anagusa mioyo na mambo hayo hubaki
katika kumbukumbu. Katika Injili tunayoitafakari Bwana Mtakatifu Luka anatupa mifano
mitatu aliyoitumia Bwana katika kupeleka jibu la Mungu Baba ni nani.
Mungu
Baba tunayemsikia katika mfano wa kwanza ni yule ambaye yu karibu nasi, ambaye anafuatilia
maisha yetu ili tusipotee na hata tukichomoka toka katika zizi basi hufanya kila aina
ya bidii kuturudisha. Kumbe Mungu Baba yuko karibu nasi kwenye familia, vituo vya
kazi na mahali pote ambapo tunapata kuishi. Ndama mmoja au shilingi moja ikipotea
basi huacha walio wengi au zilizo nyingi ili kuhakikisha moja iliyopotea inapatikana.
Ndiyo kusema Mungu Baba anataka hata mmoja wetu asipotee bali awe na uzima
wa milele. Ni tofauti na Mungu wa Mafarisayo ambaye ni kwa ajili ya wenye haki tu!
Mungu Baba ni yule ambaye hamtengi hata mmoja bali ni kwa ajili ya wote wema na wabaya.
Mpendwa
msikilizaji, mfano wa tattu ni ule wa mwanampotevu, ambaye kwa hakika katika hali
ya kawaida asingepaswa tena kufanyiwa sherehe kubwa namna ile. Lakini Baba kwa upendo
mkamilifu pasipo kuuliza ulikuwa wapi anamvika mavazi na pete ya thamani kubwa. Anatuonesha
furaha ya kurudi kundini yule aliyepotea. Inatuonesha matunda ya toba kwa awaye yote
katika maisha ya hapa duniani tukielekea mbinguni.
Baba anasema, tufanye sikukuu!
Bwana anasimulia na kuonesha moyo wa Mungu unaowaka mapendo na furaha iliyofungamana
na kusamehe na si furaha kuwaka moyoni bali hata kuifurahia furaha hiyo.
Mpendwa
msikilizaji mwanafalsafa Machiavelli aliwahi kusema “siasa ni hali ya kutokuwa mwema”
hii ni hali ambayo imeenea sasa katika ulimwengu wa leo, inajionesha katika kutotenda
haki kwa wananchi. Basi leo Bwana anataka kutupeleka upande mwingine yaani namna
ya kuwa mwema katika maisha yako! Ni kuishi na kutenda Huruma kwa wengine kama Baba
alivyomtendea mwanampotevu. Ni kuwarudisha walioenda mbali nasi karibu nasi.
Huruma
ambayo Baba anaionesha inakuwa kinyume na kaka mkubwa ambaye alikuwa amejaa hasira
kwa sababu ya kusamehewa mdogo wake kahaba aliyetumia vibaya mali ya Baba yake. Huyu
kaka mkubwa tunaweza kusema ni mwenye kutenda pasipo imani, maana imani yatupeleka
mpaka pale ambapo upendo haufungwi na sheria na mipaka ya mahesabu bali unajitoa katika
hali zote.
Basi yafaa kuangalia sisi tunayo imani au ni watendaji wa shughuli
zinazohusiana na imani? Imani si tu katika vitu vya nje bali ile ambayo hutupeleka
katika kushirikishana utajiri wa mbinguni, matendo ya kimungu, huruma ya Kimungu nk.
Mpendwa,
nikutakie safari ya mabadiliko ya kiroho ukitaka kujifunza matendo na huruma ya kimungu
daima ili kuweza kuwa daraja kwa ajili ya wokovu wa wengine.Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.