2013-10-15 07:46:03

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 23 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa


Tunaendelea na tafakari ya Neno la Mungu, tayari tukiwa Dominika ya 23 ya mwaka C Ni siku ya furaha na nderemo, Mama Kanisa atuwekea Neno la furaha, Neno ambalo kwalo Kristu anakuja na fundisho la kuta kutuondoa katika kufungwa na minyororo isiyo ya msingi kwa maisha yetu ya kikristo. Anataka tuchague jambo la msingi kuliko mambo mengine na kulitekeleza pasipo visingizio. Kwa nini Bwana anakuja na fundisho hili ambalo kwa juujuu linaonekana kwenda kinyume na utu wa kawaida. Anadai mmoja ili aweze kuwa mfuasi wa kweli lazima aachane na familia yake!

Bwana anakuja na namna hiyo akitaka kuwasaidia watu ambao walikuwa wakitaka kumfuata pasipo kujua majukumu katika kumfuasa yeye. Watu walikuwa wanafikiri kumfuata ni lelemama! Makutano walikuwa wakivutwa zaidi na miujiza pasipo kufikiria hekima ya moyo zaidi. Kwa sababu hiyo Yesu anageuka na kumwambia mmojammoja anayetaka kumfuata lazima atambue kuwa kuna msalaba wa kubeba na wala si raha na chakula pamoja na miujiza. Fundisho sasa halielekei makutano bali mtu mmojammoja. Ndicho anachokuambia wewe leo kumfuasa yeye ni shughuli nzito inayodai akili yako na uwezo wako wote.

Katika kutoa fundisho lake anakuwa mkali kidogo akisema kama mmoja hachukii wazazi wake na mke wake basi huyo hawezi kuwa mfuasi wangu. Anataka kugusa sehemu nyeti ya maisha ya mwanadamu, anagusa uhusiano ulio katika mtima wa moyo. Anataka pia kukomaza wazo la familia kubwa ndiyo Kanisa. Haondoi familia bali anatoa mwanga ili mmoja asije akafikiria familia ndio mwisho wa yote. Anataka kukuza uhuru kamili katika kumfuasa yeye ili mmoja asije akafungwa na minyororo ya mawazo ya familia. Na hivi mwisho wa yote ni yeye mwenyewe.

Anaturudisha kwenye jaribu la imani ya Ibrahimu Mungu akidai sadaka ya mwanae Isaaka. Inauma lakini Ibrahimu anatenda na anaibukia Baba wa imani na anapata zawadi kuwa mtu wa haki. Bwana akisonga mbele baada ya hilo anakuja na mifano miwili yaani inayomwandaa mtu katika kutaka kumtumikia Mungu kwa ukamilifu. Anauliza Je mmoja akitaka kujenga mnara si anajiandaa ili asije akashindwa kuumaliza na hivi akaingia katika kuchekwa na watu. Je mtu akitaka kupigana na mfalme mwingine si anaandaa majeshi yake na hivi kama anaona hayatoshi anaomba mapatano ya amani kabla?

Bwana anataka tuondokane na mshikamano wa siasa au mawazo ambayo yanavuka mipaka ya mapendo ya kimungu. Tunaitwa kushika Injili ya Mapendo kadiri ya mafundisho ya Bwana mwenyewe. Injili ya mapendo inajikita katika msalaba wa Bwana, katika kutoa kulikokupokea, kuishi unyenyekevu badala ya ubwanyenye. Hapa ndipo tunaweza kuwa wanafunzi wa Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.