Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika katika mkutano wake uliofanyika mjini Addis Ababa,
Ethiopia mwishoni mwa juma, wameendelea kupinga mwenendo wa Mahakama ya uhalifu wa
kimataifa dhidi ya ubinadamu iliyoundwa na Umoja wa Mataifa ili kuwashughulikia watu
wanaojihusisha na mauaji ya kimbari, vita na uvunjaji wa haki msingi za binadamu.
Katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa,
kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Afrika, viongozi
hao waliutaka Umoja wa Mataifa kuangalia upya mwenendo wa mashitaka dhidi ya Omar
Hassan Al Bashir wa Sudan, Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto wa Kenya.
Viongozi
wanaotuhumiwa hawapaswi kushitakiwa wakiwa bado madarakani na kwamba, Mahakama ya
makosa ya kivita imeonesha mwelekeo potofu dhidi ya Bara la Afrika, tangu ilipoanzishwa
kunako mwaka 2002 hadi wakati huu. Mahakama hii ilikuwa pamoja na mambo mengine kuhakikisha
kwamba, inalinda na kutetea haki msingi za binadamu pamoja na kuendeleza mchakato
wa upatanisho, lakini kwa bahati mbaya imegeuka kuwa ni chombo cha kisiasa dhidi ya
Bara la Afrika na viongozi wake.
Hii ndiyo hali ya jumla inayosikika kutoka
Barani Afrika. Viongozi kutoka Barani Afrika wanataka wapewe kinga dhidi ya njama
za Mahakama ya uhalifu wa kivita wanapokuwa madarakani.