2013-10-15 11:25:42

Msongamano wa magari kwenye mizani Tanzania sasa ni "Janga"


Zikiwa zimepita siku chache tangu Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda aagize malori yarejee kutumia utaratibu wa zamani wa kupima mizigo kwenye mizani, hali bado ni tete kutokana na misururu mikubwa iliyokuwepo Jumapili, Oktoba 13, 2013 kwenye mizani ya Mikese na Kibaha.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia msururu wa malori na mabasi zaidi ya 105 kwenye mizani ya Mikese mkoani Morogoro bila kujali idadi ya magari madogo yaliyokuwepo kwenye foleni ya kutoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro.

Mashuhuda waliokuwepo kwenye mizani ya Mikese walisema kuwa mizani inayopima magari ya kutoka Morogoro imeharibika tangu jana ndiyo maana inatumika mizani ya upande mmoja tu (wa kutoka Dar es Salaam). Kulikuwa na dalili za mafundi kufanya matengenezo kwenye maegesho ya mzani huo ambapo malori na mabasi huwa yanasimama.

Katika mizani ya Kibaha mkoani Pwani hali nako haikuwa shwari sana licha ya kuwa mizani ya pande zote mbili ilikuwa ikifanya kazi. Magari ya kutoka Dar es Salaam peke yake yalikuwa zaidi ya 90 bila kuhesabu magari madogo yaliyokuwa kwenye foleni hiyo ya kuelekea Morogoro.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu alitengua uamuzi wa awali wa Serikali uliotolewa Oktoba Mosi, 2013 na Waziri wa Ujenzi ambao ulikuwa ukiondoa msamaha wa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubalika kisheria.

Vilevile, Waziri Mkuu aliamua kuunda kamati maalum kamati ambayo aliipa muda wa mwezi mmoja na kuitaka ikutane na wadau ambao ni Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TATOA) na Chama wa Wamiliki wa Mabasi yaendayo Mikoani (TABOA) ili kupata ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza.

“Natoa kipindi cha mwezi mmoja kwa wizara husika na wadau hao kukamilisha kazi hiyo. Katika kipindi hicho cha mpito, utaratibu ulikuwepo awali kabla ya tangazo la tarehe 01 Oktoba 2013 lililotolewa na Wizara ya Ujenzi, utaendelea kutumika,” alisema.

"Kwa kuwa bado kuna mgogoro kati ya Wizara ya Ujenzi, Wasafirishaji wa malori na mabasi kuhusu utekelezwaji wa kanuni 7(3), ambao wanasema haitekelezeki kirahisi, naiagiza Wizara ikutane na wadau. Wakae na kujadili namna bora ya kutekeleza kanuni hii, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waunde timu ya wataalamu ambao watakutana na wawakilishi wachache wa TATOA na TABOA ili wapitie kanuni hizi kwa lengo la kupata mwafaka," alisema Waziri Mkuu.








All the contents on this site are copyrighted ©.