2013-10-15 10:28:45

Jihadharini na matapeli wakati wa Ibada ya kuwatangaza watakatifu Yohane Paulo II na Yohane wa XXIII


Mama Kanisa anatarajiwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu Jumapili ya tarehe 27 Aprili 2014, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa na bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Vatican inapenda kuwatangazia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, katika Ibada ya Misa ya Siku hiyo, hakutakuwepo na tiketi maalum kwa ajili ya kuhudhuria Ibada hiyo. Kila mtu atakuwa huru kuingia katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na viunga vyake kadiri ya nafasi itakavyoruhusu.

Vatican pia inawataadharisha watu wasijekujikuta wanatapeliwa na makampuni ya kitalii kwa kuwatoza fedha kwa ajili ya kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwatangaza Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu.

Mchezo kama huu umewahi kufanyika katika matukio kama haya. Vatican inapenda pia kuwajulisha waamini na watu wenye mapenzi mema kwamba, tiketi zinazotolewa kwa ajili ya kushiriki kwenye Katekesi na Ibada zinazoendeshwa na Baba Mtakatifu ni bure na wala haziuzwi.








All the contents on this site are copyrighted ©.