Taifa la Liberia , Ijumaa lilikuwa msitari wa mbele kuadhimisha Siku ya Kimataifa
ya Mtoto wa Kike. Kwa ajili hiyo, Rais Ellen Johnson-Sirleaf wa Liberia, aliitangaza
siku hiyo ya Kimataifa kwa ajili ya mtoto wa kike, rasmi kama Sikukuu ya Kitaifa
lakini lakini ya kikazi. Hapo siku ya Jumatano Wizara ya mambo ya nje ya nchi
hiyo ilitoa mwito kwa mashirika yote ya kitaifa na kimataifa yakiwemo mashirika kama
vile Shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, na Plan Liberia, pamoja
na wizara mbalimbali za serikali ya Liberia, kuungana na Wizara ya Jinsia na Maendeleo
ya nchi hiyo ili kuandaa Khafla mbalimbali kwa ajili ya kuadhimisha sikukuu hiyo ipasavyo. Rais
Sirleaf anasema kwamba kuadhimisha siku hiyo ya kimataifa kwa ajili ya wasichana kunaenda
sambamba na azimio la Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly Resolution
66/170) la Disemba 19, 2011 lililoikumbatia siku ya Oktoba 11 kama “Siku ya Kimataifa
kwa ajili ya Mtoto wa Kike” Maadhimisho ya siku hiyo mwaka huu (2013) yanalengo
la kuangazia mada ya “Mbinu mpya kwenye elimu na majifunzo ya wasichana”. Maadhimisho
hayo pia yananuia kujadiliana juu ya mbinu mkakati kwa ajili ya uboreshaji wa elimu
ya wasichana nchini Liberia, na kuzindua Ripoti maalum kuhusiana na Mtoto wa kike
nchini humo. Ujumbe uliotoa Mwito wa kuadhimisha siku hiyo nchini Liberia pia umesema
maadhimisho hayo nimwendelezo wa yale yaliyojiri kwenye kongamano lililofanyika nchini
humo mwezi Julai 2013. Kongamano hilo lililohudhuriwa na wasichana kutoka pembe zote
za Liberia lilijadili mbinu za kuwajengea wasichana uwezo wa kujadili na kutekeleza
maazimio ya kumwendeleza mtoto wa kike nchini humo. Maadhimisho ya Siku ya kimataifa
ya Mtoto wa Kike yanatoa fursa kwa Liberia kutazama upya haki za wasichana na changamoto
za kipekee zinazowakumba watoto wa kike ndani ya jamii kote duniani, na hivyo kuonyesha
mshikamano na jumuiya ya kimataifa katika jitihada za kuthamini mchango wa wasichana
kwenye jamii. Ni fursa pia ya kutafuta mbinu muafaka za kuwekeza kwa ajili ya kuwawezesha
watoto wa kike ki maisha na kupinga kabisa kuwabagua, na uonevu wowote wa kijinsia
dhidi ya wasichana.