Msingi wa amani unaanzia kwenye asili takatifu na ya kimungu ya binadamu. Nayo hati
ya kichungaji juu ya amani duniani "Pacis In Terris" inaazimia kuwakumbusha
binadamu asili hiyo ya binadamu, ya jamii na hata ya uongozi na madaraka. Ni asili
hii Takatifu ambayo inawaashiria watu binfsi, wana familia, vikundi mbalimbali kwenye
jamii na hata mataifa kufanya juhudi za kuendeleza mahusiano ya haki na mshikamano.
Ndivyo
anavyosema Baba Mtakatifu Francisko kwenye maadhimisho ya miaka hamsini ya hati ya
kichungaji Pacis In Terris.
Kama Yesu Kristo mwenyewe alivyofanya, anasema
Baba Mtakatifu, kila mmoja anao wajibu wa kujenga amani kwa kuishi kwa haki, ukweli
na upendo, huku akichangia, kwa uwezo wake, maendeleo ya kina ya binadamu, ndani ya
mantiki ya ushirikiano na mshikamano halisi.
Ukumbusho wa Hati ya Pacis In
Terris umefanyika muda mfupi baada ya kutangazwa siku ya kumtawadha hadhi ya utakatifu,
Mwenye Heri Yohanne wa XXIII, Baba Mtakatifu aliyeichapisha hati hiyo mnamo tarehe
11/04/1963.
Ulikuwa ni wakati wa vita baridi, anasema Papa Francisko, na dunia
nzima ilikumbwa na kilio kwa mateso yaliyowafika watoto kwa wazee. Ni wakati huo ambapo
Papa Yohanne wa XXIII alipotoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchunguza dhamira na
kumwelekezea Mungu maombi ya amani
Hiki ni kilio kilichoelekezwa kwa watu
waliokuwa kwenye madaraka, lakini zaidi kilikuwa kilio kilichoelekezwa mbinguni, kwa
Mungu mwenyewe. Kutokana na mwito huo wa Papa Yohanne wa XXIII kulianzishwa mjadala
mrefu na mgumu kati ya pande zilizokuwa zikizizana. Mwito huo ulitoa uwanja wazi kwa
ajili ya majadiliano ya kina, mjadala ambao hatimaye uliendelezwa na Baba Mtakatifu
aliyefuatia, Mwenye Heri yohanne Paulo II. Mbegu za amani alizopanda Mwenyeheri
Yohanne wa XXIII zimezaa matunda, anasema Papa Francisko.
Baba Mtakatifu anaendelea
kuwaalika wote kutafakari ikiwa kweli mafunzo ya pacis In Terris yana maana ndani
ya kizazi cha leo, huku akijiuliza kama maneno AMANI, Mshiklamano na HAKI yana maana
tu ndani ya kamusi au hata pia kwenye maisha ya kila siku ya kila mwanadamu. Changamoto
iliyoko, anasema Baba Mtakatifu, ni kwamba hakuwezekani kuwa na amani ya kweli na
ulinganifu kati ya watu, ikiwa hakuna kujishughulisha, kwa udi na nta, katika kujenga
jamii bora zaidi yenye kuzingatia haki na mshikamano; jamii inayoshinda ubinafsi,
umimi, na mafao ya vikundivikundi, katika kila hali; Jamii inayojua kumthamini kila
mwanadamu, aliye na asili Takatifu, ya kimungu; Jamii inayowakumbatia watu wote.