2013-10-04 08:27:47

Kanisa niTakatifu asema Papa Francisko


Kanisa lina sifa ya utakatifu, sifa ambayo imejidhihirisha tangu enzi za wafuasi wa kwanza wa Yesu, ambao wanaitwa kwa kifupi, watakatifu, kwani walikuwa na uhakika kamili kwamba ilikuwa ni kazi ya Mungu, Roho Mtakatifu, ambaye alikuwa akilitakatifuza Kanisa. . (Mat. 9,13.32.41; Rm 8,27; 1 Cor 6,1).

Kwenye Katekesi yake Jumatano hii Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waliokuwa wakimsikiliza kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatikani kwa kuwauliza ni vipi utakatifu wa Kanisa unajidhihirisha ndani ya safari yake tangu mwanzo wake, kuna magumu, shida na hata nyakati zenye giza? Kanisa lenye kuongozwa na binadamu, wenye dhambi linawezaje kuwa takatifu? Alihoji Papa.

Akirejelea barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso, (Ef. 5:25-26), Baba mtakatifu anasema kwamba Mtume Paulo akiongelea juu ya mahusiano ya kifamilia, aliwataka Waefeso wapendane kama Kristo alivyolipenda Kanisa lake – mpaka kujitoa kwa ajili yake, ili aweze kulitakasa. Maana yake ndio nini hasa?

Kanisa ni Takatifu kwani linatoka kwa Mungu, na kwamba Kristo, aliye Mungu, ameunganika na Kanisa kwa namna ambayo haiwezi kujitenga, na kwamba kanisa linaongozwa na roho Mtakatifu ambaye hutakatifuza, husafisha na kupyaisha, anaelezea Papa. Ni utakatifu usiotokana na uwezo au mastahili ya binadamu, bali ni tunda la Roho Mtakatifu na mapaji yake.

Anaendelea kusema Baba Mtakatifu kwamba japo Kanisa linaongozwa na binadamu, haimaanishi binadamu hao ni kamili, bali hata wao wanaalikwa kuongoka, kuhuishwa na kutakatifuzwa na Mungu mwenyewe.

Papa Francisko ameonyesha masikitiko kwamba historia inaonyesha kwamba kunao watu waliofikiria kwamba Kanisa ni la wale walio tayari wema na wanyofu tu, ambao iliwapasa kujitenga na wengine, wasio wakamilifu! Mtazamo huo, anasema Papa, unaenda kinyume na sifa ya Kanisa takatifu, ambalo huwapokea hasa wakosefu na wale walio mbali zaidi.

Kanisa Takatifu huwaalika wote kupokea huruma, upendo na na msamaha wa Mungu anayewawezesha watu wote kukutana naye na kutembea naye katika utakatifu. Papa ametoa mwito kwa wote wenye kujisikia wakosefu kufahamu kwamba Mungu anawapenda na wasione aibu ya kujiunga na Kanisa bali wawe na unyenyekevu wa kumkaribia Mungu katika hali zao halisi za kimaisha.

Kama mwana mpotevu, anasema Papa, wakati mtu anapopata nguvu ya kujirudi, hushangazwa hata yeye na mapendo ya Baba aliye daima tayari kumpokea, kumbusu na kumwandalia sherehe. Baba Mtakatifu analichangamotisha Kanisa kuwa mahali ambapo kila mmoja, aliye thabiti na hata aliye mnyonge zaidi, anaweza kujisikia nyumbani; mahali ambapo wote wanapata nafasi ya kujipyaisha, wakiwa wametakatifuzwa na upendo wake Mungu. Kanisa linatoa nafasi sawa kwa wote kuweza kutembea katika utakatifu; linawapa wote nafasi ya kukutana na kristo katika Sakramenti na hasa kwenye sakramenti za Upatanisho na Ekaristi. Kanisa linawasilisha neno la Mungu na Upendo wake kwa jumla.

Ni mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa wote kutokuwa na hofu bali kumwangalia Mungu Mwenyewe na kujiachilia mikononi mwake yeye tu awezaye kutakatifuza.








All the contents on this site are copyrighted ©.