2013-09-27 15:41:21

Wito wa watawa wa AOSK na ACWECA ni kuendelea..


Baraza la Mashirika ya watawa wa kike nchini Kenya (AOSK) likishirikiana na Baraza la mabaraza ya mashirika ya watawa wa kike Afrika Mashariki na ya Kati (ACWECA) siku ya Jumatano (25/09/2013) waliandaa maandamano ya sala kwa ajili ya waathirika wa shambuliza la kigaidi lililofanyika kwenye kituo cha maduka cha Westgate, kilichoko jijini Nairobi, Kenya.

Ujumbe uliotumwa kwenye vyombo vya habari na ambao uliwekwa sahihi na mwenyekiti wa AOSK, Sr. Margaret Aringo FSJ ulisema kwamba watawa wa kike nchini Kenya na kote Afrika Mashariki na ya Kati walihuzunishwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyolikumba taifa la Kenya.

Watawa hao waliowekwa wakfu kwenye Kanisa Katoliki wanasema kwamba maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu; na kwamba umoja na upendo kati ya watu wa Mungu ni vitu vya muhimu katika kushuhudia haki na ukweli, tunu ambazo zinaambatana na roho wa Mungu kwa watu wake.

Watawa hao waliwashukuru wote walioonyesha mshikamano wao na kutoa huduma muhimu kwa waathirika, wakati wa mkasa wa Wastegate. Maafisa wa usalama, Mahospitali, watu binafsi na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla walichangia kwa hali na mali wakati wa janga hilo la kitaifa.

Ni mwito wa watawa wa AOSK na ACWECA kuendelea kuwaombea waathirka wa mkasa huo na wote ambao wanaendelea kuteseka sehemu mbalimbali za dunia kutokana na mashambulizi ya kigaidi.











All the contents on this site are copyrighted ©.