2013-09-27 15:21:59

Papa asema, Mkristu wa kweli huyapokea mateso kwa furaha


Uthabiti wa imani ya Mkristo ,huonekana katika uwezo wake wa kupokea kwa furaha na uvumilivu, majaribu, madharirisho na mateso katika maisha ya kila siku. Papa Francisko alieleza hili wakati akitoa tafakari juu ya maisha ya imani, wakati akiadhimisha Ibada ya Misa katika kanisa dogo la Mtakatifu Marta , mjini Vatican mapema Ijumaa hii. Papa kwa mara ingine alitazama majaribu yanayopambana na ustawi wa kiroho , yanayozuia Mkristu kumpenda Kristo kwa moyo wake wote

Homilia ya Papa imeonya hatari ya msimamo nusunusu katika imani ,imani isiyotaka kujiweka dhahiri badala yake imejibaza nyumanyuma katika kona, bila kujitokeza dhahiri, ambamo muumini huyo daima kichinichini anakuwa na kisingizio na udhuru. Papa alieleza kwa kutazama somo la Injili ya Luka, kifungu ambapo Yesu anawauliza wanafunzi wake, “watu wanasema Yeye ni Nani”, Na kisha akawageukia , na ninyi mwasema Mimi ni nani. Petro alijibu :Wewe ndiwe Kristu, Mwana wa Mungu.

Papa alielekeza swali hilo kwa waliokuwa wakimsikiliza akiuliza, Kwako wewe wasema Yesu Kristu ni Nani? Je unaamini ni Bwana wa maisha yako, Nabii mwema , Mwalimu mwema anaye ufanya moyo kuwa na furaha na mema mengi? Na je unasadiki kuwa ni Mtakatifu na ukweli wote, yule anayetembea nawe katika maisha yote , anayekusaidia kusonga mbele na kuwa mtu mwema ?

Papa aliendelea kusema, kwa jibu la Petro, Yesu anawataka wasimwambie mtu yeyote, na kuwatangazia mateso yake, kifo chake na ufufuo wake. Na kama ilivyoelezwa katika Injili ya Mtakatifu Mathayo , Petro anasema, hili kamwe haliwezi kutokea! Papa anasema, Petro anaonekana kutishika, na kufadhaika, kama ilivyo pia kwa Wakristo wengi ambao wanapopatwa na matatizo na mateso husema kamwe hili haliwezi kunitokea, kwa kuwa mimi ni muumini aminifu kwa Kristu, akisahau kwamba kumfuata Kristu ni kuifuata njia ya mateso ya kudharirisha na kifo.

Papa aliendela kutafakari imani ya Muumini na ustawi wake wa kiroho akisema, tangazo la Kristu kwa wafuasi wake juu ya mateso , kifo na ufufuko ni tangazo linaloonyesha njia ya ustawi wa kiroho.Alisema tuna kila msaada, Yesu Kristo, Kanisa, Sakramenti, Bikira Maria, yote yakiwa ni kazi nzuri kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, na hivyo Mkristu anajiona amekamilka. Lakini haya yasitufanye kusahau kuzingatia kwamba bado tunatakiwa kusimama imara katika kupambana na mawimbi yanayoambatana na majaribu ya mateso na kifo cha aibu kama ilivyokuwa kwa Kristu mwenyewe. Kashfa hii ya msalaba anasema Papa, huzuia Wakristo wengi kushikilia imani thabiti.

Lakini Mkristo wa kweli anaye Roho Mtakatifu anayemwezesha kuyapokea majaribu na matatizo kwa furaha na uvumilivu na tena kwa unyenyekevu kama tunavyojifunza katika shuhuda nyingi za maisha ya Wenye Heri na Watakatifu. ..Mkristu hupata ushupavu huu kwa kuwa karibu na Yesu, daima akifanya hija yake ya maisha katika tumaini la maisha lililotangazwa na Yesu.








All the contents on this site are copyrighted ©.