2013-09-27 08:11:53

Neno la Mungu ni taa ya shughuli zote za kichungaji.


Neno la Mungu huoingoza imani na shughuli za kibinadamu na huwapa waumini njia muafaka ya kufuata wakiongozwa na Roho Mtakatifu kwenye maisha yao ili kuweza kuyaishi mafumbo ya Kristo kama mwito wao wa Kikirsto.
Kutokana na mwelekeo huo, Kanisa halina budi kuwaunda waumini ili waweze kuliishi na kuligawanya neno la Mungu kama tunu ya maisha ya Kikristo. Kanisa pia linahitaji kuendeleza maundo ya kina kwa ajili ya mashirika ya kibiblia na makundi mengine yenye kuwajengea waumini uwezo wa kulitafakari na kulieneza neno la Mungu.
Haya yamebainika kwenye ujumbe uliotolewa mwishoni mwa kongamano la Kituo cha Kiroho cha Biblia kwa ajili ya Afrika na Madagascar, BICAM, cha mjini Lilongwe, Malawi. Kongamano hilo limefanyika kuanzia tarehe 17 hadi 23 mwezi Septemba, 2013 kwenye Seminary kuu ya Kachebere jimbo kuu la Lilongwe. Mada ya kikao hicho imekua ni: Kuliachia neno la Mungu Kuziongoza shughuli zote za kichungaji.
Kongamano hilo lilikubaliana kwamba Utume wa kibiblia ni chombo muhimu katika kukabiliana na ongezeko la makundi ya kidini na watu wenye kutafsiri Biblia visivyo. Hata hivyo, utume huo wa Biblia haujaenea sana katika nchi nyingi barani Afrika. Pia ilionekana kwamba kukua kwa siasa za Kiislam, itikadi kali na uongozi mbaya barani Afrika ni changamoto kwa tamaduni za Kikristo.
Kongamano hilo liliafikiana kukuza ushirikiano kati ya mabaraza ya maaskofu Katoliki na mashirika ya kitume baran Afrika, pamoja na kuwajengea uwezowa kuendesha shughuli zao kitaaluma na kiaminifu wakurugenzi wa utume wa Biblia kitaifa na wa kikanda.
Ni muhimu pia kufikiria na kutafakari pamoja juu ya changamoto mbalombali zinazoikumba jamii ya leo na kushirikiana kikamilifu katika kuendeleza utume huo, kwenye jumuia ndogondogo za kikristo, na kuwahusisha hasa vijana ambao ni wanakumbana na changamoto na maswali chungu nzima kuhusiana na maisha ya Kikristo.
Vyombo vya habari na tecknologia mpya pia vimemulikwa na kongamano hilo kama uwanja mpya wa uinjilishaji. Hivyo ni muhimu Kanisa kutumia teknologia hizo ambazo hutumiwa sana na vijana, hata katika kufundishia neno la Mungu.
Nao waandishi wahariri nao wauzaji wa vitabu vya Kikatoliki hawana budi kushirikiana katika kuchapisha na kueneza Biblia na Vitabu vingine vyenye kuhusiana na Biblia, kama vile Biblia na kalenda za Kiliturgia.
Kongamano hilo la juma moja limehudhuriwa na washiriki kutoka mabaraza ya maaskofu ya Afrika ya Kati, ACEAC na ACERAC; Afrika Masahriki, AMECEA; Afrika Magharibi, RECOWA; na Afrika ya Kusini na Madagascar, IMBISA. Pia Baraza la Maaskofu la Misri, AHCE, liliwakilishwa kwenye kikao hicho.
Wengine walioshiriki walikuwa maaskofu wenye kushughulika na utume wa Biblia kitaifa au kikanda barani Afrika, na wawakilishi wa Mapadri, na mashirika ya kitawa na ya kilei.
Washiriki wa Kongamano hilo wanasema kwamba wameuona mkono wa Bwana ukifanya kazi kwenye mkutano huo na wanawashukuru watu binafsi na mashirika kama vile Church in Need na Missio, na shirika la kipapa la Cor Unum, walioshirikiana ili kuufanikisha mkutano huo.










All the contents on this site are copyrighted ©.