SECAM Kukutana na Viongozi wa kiserikali wa Afrika mjini NY
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM likishirikiana
na mashirika ya kimataifa ya kikanisa yenye kuhusika na maendeleo ya jamii, limepanga
kukutana na baadhi ya viongozi kutoka nchi za Afrika wakati wa Mkutano Mkuu wa 68
wa Umoja wa Mataifa unaofanyika mjini New York kuanzia tarehe 23 hadi 25 Septemba
2013. Lengo la mkutano huo ni kujadiliana pamoja na viongozi hao wa kitaifa juu ya
mikakati kwa ajili ya maendeleo endelevu barani Afrika kwa siku za usoni.
Maaskofu
wa SECAM wanauona huu kama wakati muafaka wa shirikisho hilo kufanya mazungumzo ya
ana kwa ana na viongozi watakaokuwa wanayawakilisha mataifa ya Afrika kwenye mkutano
huop wa New York. Mazungumzo hayo yanawania kumulikia maswala yanayojitokeza katika
jitihada ya kutimiza malengo ya millenia kwa ajili ya maendeleo (MDG), na mikakati
ya maendeleo ya bara baada ya mwaka 2015.
Maaskofu wanakubaliana kwamba ni
muhimu kutoa kipaumbele cha kwanza katika kujenga uwezo wa wana wa bara la Afrika
kuweza kujiendeleza wenyewe, maendeleo ya kudumu na wala sio maendeleo ya msimu, au
yenye kuwafaidi watu wachache huku watu wengi wakiendelea kuhangaika bila ya matumaini.
Wanasema maaskofu hao kwamba kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba maendeleo endelevu
kwa ajili ya bara Afrika linatia maanani maswala ya maadili, hadhi ya binadamu na
maslahi ya watu wote hasa wale walio wanyonge zaidi na wenye kusukumizwa pembezoni
mwa jamii.
Baadhi ya marais watakaokutana na wawakilishi wa SECAM ni pamoja
na Ellen Sirleaf Johnson, Rais wa Liberia na Mwenyekiti wa kamati ya juu ya viongozi
wa serikali wa Umoja wa Afrika. Wengine ni Jacob Zuma wa Afrika Kusini, John Mahama
wa Ghana, Haile Mariam Desalegu wa Ethiopia na mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika,
Daktari Nkosazana Dlamini-Zuma.
Mashirika ya kimataifa yatakayowakilishwa kwenye
majadiliano hayo ni pamoja na CAFOD, CIDSE, Trocaire, Caritas Internationalis, na
Cordaid, Manos Unidas, Misereor na SCIAF.