2013-09-23 15:29:46

Kila mmoja na amtazame mwingine kwa macho ya huruma ya Mama Maria – Wito wa Papa Francisko ziarani Cagliari Sardinia.


Jumapili (22 Septemba 2013)Papa Francisko alifanya ziara ya kichungaji katika mji wa Cagliari kisiwani Sardini , Kusini mwa Italy. Kati ya mengine aliyoyafanya ni kuongoza Ibada ya Misa katika Madhabahu ya Mama Yetu wa Bonaria na kuhutubia makundi ya watu mbalimbali, mkusanyiko wa hadhara, vijana na Masista wamonaki wa ndani. Kwa Papa Francisko , ziara hii inatajwa kuwa na umuhimu wake, kwamba, mji Buenos Aires wa Argentina, nyumbani kwake, una asili ya jina hilo la Mama yetu wa Bonaria .

Katika homilia yake, Papa Francisko, alitaja nia ya ziara hiyo kwamba, alipenda kushirikishana na wakazi za mji wa Cagliari na kisiwa chote cha Sardinia, hali zote za furaha, matumaini , juhudi, ahadi, maadili na matarajio ya kisiwa hicho, na pia kuwatia nguvu mpya katika imani. Pia alizungumzia mambo mengine hasa matatizo ya kiuchumi, kipeo cha ajira na ukosefu wa uhakika wa kazi kuendelea kuwepo.

Papa Francisko alisisitiza ushirikiano aminifu kwa kila mtu kwamba ni muhimu, kuandamana na dhamira safi za viongozi wa taasisi zote hata hata ndani ya Kanisa, wakizingatia haki za msingi za watu na familia. Hivyo kuunda umoja na udugu zaidi kwa watu, kama familia moja . Ni kuhakikisha haki ya kufanya kazi kwa wote kwa ajili ya kuleta nyumbani ujira, ambao unampa mtu mkate wake wa kila siku. Papa alisisitiza, mkate huo hupatikana kwa kufanya kazi kisha kulipwa ujira.

Papa aliendelea kusema, “ nimekuja Cagliari kuwa pamoja nanyi, kutoa heshima zetu na kujiweka chini ya usimamizi wake Mama Yetu Maria, Mama wa Mungu Mwana, ambaye kwa mamia ya miaka , watu wa Sardinia, wamejiweka chini ya ulinzi wake, Mama Yetu ya Bonaria”. Papa kisha aliwasisitiza watu wa Sardinia kuendelea Ibada mara kwa mara, kwa Mama huyu, wakijiweka chini ya ulinzi wake. Alisema “kamwe tusichoke kupiga hodi kwenye mlango wa Mungu, tukiyapeleka maisha yetu yote , kila siku kwa Roho wa Mungu kupitia kwake Maria”!

Mwisho Papa Francisko alisema, niko Cagliari, kukutana uso kwa uso na macho ya Maria, ambaye katika umama wake kwa wana wake, mna mwangwi wa upendo wa Mungu, Baba wa watu wake, na mtazamo wa upendo ambao Yesu aliukabidhi kwa Mtakatifu Yohane kwa Maria katika mguu wa Msalaba. Papa alieleza hayo kwa kuirejea Injili ya siku iliyosomwa na kusema, na "tumwombe Mama Maria, atuangalie kwa macho yake ya huruma ili tupate pia sisi kukutana na Baba wa upendo".

"Maria , hufundisha mtazamo ule wenye kutatafuta kukaribishwa, kuongoza na kulinda". Kisha Papa Francis alitoa mwaliko kwa kila mmoja apende kujifunza kumtazama mwingine kwa macho haya ya kimama ya Maria, yanayo tuwezesha kuwaona waliotelekezwa, wahitaji zaidi, wagonjwa na wale wasiokuwa na kitu, wale ambao bado hawajamjua Kristu , vijana walio kosa ajira,na wenye matatizo. Yote na tuyatolee kwa Mama Yetu wa Bonaria, ili atusindikize katika njia yote ya maisha.









All the contents on this site are copyrighted ©.