Mitandao ya kijamii imeonyesha kuvifuatilia kwa karibu Vyombo vya habari vya Kanisa
Katoliki kwenye siku za hivi karibuni. Wengi wanasema hii ni kutokana na watu wengi
kuvutiwa na Baba Mtakatifu Francisco ambaye habari zake huchapishwa kwanza kwenye
vyombo hivyo. Vyombo kama gazeti la kila siku lenye kuchapishiwa mjini Roma la Osservatore
Romano, lililoanzishwa mnamo mwaka 1861, na Radio Vatican, ambayo imekuwa ikirusha
matangazo yake hewani tangu mwaka 1931 vimeonyesha ongezeko la watu wenye kuvifuatia
kwa karibu kwenye mitandao ya kijamii kama vile Tweet na facebook.
Naye Baba
Mtakatifu Francisko anaendelea kuwa kiongozi anayefuatiliwa zaidi kwenye mtandao wake
wa Tweet ambapo ndani ya miezi sita ya wadhifa wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro
tayari ana zaidi ya wafuasi millioni tisa na laki tatu, na zaidi ya watu millioni
sabini hupata kusoma ujumbe wa Baba Mtakatifu kila siku kutokana na wenzao kuuweka
ujumbe huo kwenye kurasa za mitandao yao. Nao mtandao rasmi wa mawasiliano ya Vatican
sasa una zaidi ya wasomaji milioni kumi, laki mbili na sabini kutoka kote ulimwenguni
wanaousoma wakitumia lugha mbalimbali za dunia.
Hii ni wazi ishara ya uinjilishaji
mpya ya kizazi kipya, kwenye mazingira mapya ya mawasiliano ya kijamii yanayoendelezwa
na utumiaji wa teknolojia za kisasa, anasema Askofu Mkuu Claudio Celli, rais wa Baraza
la kipapa kwa ajili ya mawasiliano ya kijamii.
Akizungumza mjini Roma na gazeti
la kila siku la Osservatore Romano siku moja kabla ya kuanza mkutano mkuu wa Baraza
la Kipapa la mawasiliano ya kijamii, Mons. Claudio Celli amesema kwamba uwezo wa Baba
Mtakatifu Francisko wa kuwasiliana na watu wa tabaka mbalimbali na kuweza kueleweka
nao, ni namna mpya ya kuendeleza mawasiliano ya kijamii ndani ya Kanisa.
Anasema
Askofu Mkuu Celli kwamba mambo manne yanajionyesha wazi kwenye staili ya mawasiliano
ya Papa. Kwanza kabisa Baba Mtakatifu anatumia lugha ya kawaida, inayoelewekana mtu
wa kawaida kwa urahisi. Pili anao ujumbe ambao unaigusa mioyo na dhamiri za watu kwani
unagusia hasa mateso ya watu na safari ya ndani, mwaliko kwa kila mtu kujitafiti mwenyewe.
Papa anafahamu kile kilischo moyoni na hivyo kumfanya kupendwa na watu wengi hata
wale waio amini, na watu wa dini nyingine za kikristo na zisizo za Kikristo.
Kitu
cha tatu kinachomfanya Papa Francisko kuwa kipenzi cha wingi, anasema Mons. Celli,
ni namna yake ya kujieleza: Papa Francesco haongei tu, bali hutumia ishara zenye kuonyesha
utajiri wa kile anachokizungumzia, kitu ambacho kinatokana na utajiri wake wa kiroho.
Na mwisho kabisa, Papa anajua kugusa fikira na hisia za watu hata kupitia
kwa lugha ya mafumbo, lugha ambayo hutoa ujumbe husika zaidi hata ya maneno. Yeye
hutumia sentesi rahisi kuelezea hata dhana zisizo rahisi hata kidogo. Mfano utakaokumbukwa
ni ule wa alioutoa kama mwaliko kwa mapadri na Maaskofu kuwa wachungaji wanaoijua
hata harufu ya kondoo wao.
Wakati Baraza la Kipapa kwa ajili ya mawasiliano
linafanya mkutano wao mkuu kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21, Septemba 2013, rais wa
Baraza hilo anasema papa Francisko anatoa changamoto kwa Kanisa kuukumbatia mwuono
mkubwa wa kusafiri kwa pamoja na jumuiya ya binadamu kwenye safari ya maisha ya hapa
duniani. Mawasiliano yawe ni njia ya Mama Kanisa kukutana na wanae, kuwa karibu nao
na kujadiliana kiaminifu katika kukumbana na changamoto za kila siku katika kuishi
ukweli wa imani na maisha matimilifu.
Kwenye mkutano wake, Baraza la Kipapa
kwa ajili ya mawasiliano ya Kijamii litaangazia namna mpya ya kuwasiliana inayoonekana
kwenye maisha ya papa Francisko. Hili litafanyika ndani ya mada ya mkutano huo ambayo
inalenga kuangazia Mitandao ya Mawasiliani na Kanisa.
Mada hii imetokana na
changamoto iliyotolewa na baba Mtakatifu mstaafu Benedetto XVI kwenye ujumbe wake
wa mwisho juu ya siku ya mawasiliano duniani ambapo aliongea kwa kirefu juu ya mitandao
hiyo, na kuchangamotisha uwepo wa Kanisa kwenye mtandao wa internet, fursa mpya kwa
ajili ya uinjilishaji.