2013-09-19 08:55:29

Mamia ya vijana washiriki adhimisho la Siku ya Kimataifa ya Amani


Mamia ya watu vijana, Jumatano walikusanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya amani , chini ya Mada: Elimu kwa ajili ya amani . Tarehe rasmi ya adhimisho hili kwa kila mwaka, ni 21 Septemba , na iliwekwa kwa lengo la kupata muda wa kutafakari kwa makini zaidi, manufaa ya amani badala ya migongano, na hivyo kutoa wito kwa jumuiya na jamii nzima duniani ipende amani na kusitisha ghasia zote.

Vijana waliokusanyika katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa walipata muda wa kushirikishana uzoefu katika kazi kwa ajili ya amani katika jumuiya zao duniani kote.

Sherehe hizi zilizinduliwa kwa mlio wa maalum wa Kengele, iliyopigwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kuashiria amani, na pia kama sehemu ya kuwakumbuka waliouawa na walio nusurika katika vita, pamoja na kuchagiza uwekaji chini silaha pale ambako vita vinaendelea. Ni mlio wa kengele ya amani, na wimbo wa amani.

Redio Umoja wa Mataifa imeripoti kwamba, wakati wa tukio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, alisema, siku hii ni siku ya kutafakari na kusisitiza imani katika maisha yasiyoandamana na ghasia, pamoja na kutoa wito wa kusitisha mapigano kote duniani. Akitrejea kauli mbiu ya mwaka huu kama "Elimu kwa ajili ya amani", Bwana Ban amesema elimu ndiyo silaha yenye nguvu zaidi. Na kila mtoto anastahili kupata elimu, ili ajifunze maadili yatakayokuza jamii zenye kuvumiliana na kuheshimu tofauti za watu wengine wanaoishi nao.

Katika Siku hii ya kimataifa ya amani, tuahidi kufundisha watoto wetu thamani ya kuvumiliana na kuheshimiana. Tukiipa elimu kipaumbele, tunaweza kupunguza umaskini na kutokomeza njaa, ili tuweze kujenga jamii zenye nguvu na bora zaidi kwa ajili ya wote.

Naye rais mpya wa Baraza Kuu John William Ashe, amesema hafla ya kupiga kengele ya amani ni muhimu kukumbusha majukumu ya Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha ulimwengu wenye amani zaidi.

Tunapoisikia kengele hii ikilia, tukumbuke kuwa ni Umoja wetu wa Mataifa ndio ulioiweka siku hii ya kimataifa ya amani, katika kuzifanya nchi zote wanachama kuitambua na kutafakari kuhusu umuhimu wa amani, katika ulimwengu ambao umejaa mifano ya kila siku ya umwagaji damu, ghasia na vita. Ni siku ambayo tunajitoa kushirikiana kuendeleza amani.








All the contents on this site are copyrighted ©.