Kanisa lenye kujitenga na ulimwengu na mazingira yanayolizunguka si kanisa la Kimissionari.
Na ukweli lazima uwe kiini cha mafundisho yote ya kanisa licha ya mazingira yanayolizunguka.
Upendo na huruma ya Kikristo vinadai daima kuutangaza ukweli kwani bila huo Kanisa
linaacha kuwa kanisa. Haya ndiyo mawazo yaliyojitokeza kwenye tafakari ya Askofu
Mkuu wa Dublin, Ireland, Mons. Diarmuid Martin alipokuwa akizungumzia wito na wajibu
wa vyombo vya habari vya Kikatoliki nchini humo. Hii ilikuwa ni fursa kwake Askofu
Mkuu Martin kuyamulikia maswala mawili ya uinjilishaji mpya, ambayo ni UJUMBE, na
namna ya kuendeleza uinjilishaji mpya nchini Ireland. Habari zilizochapishwa kwenye
gazeti la kila siku la L’Osservatore Romano linalochapishwa mjini Roma, linamnukulu
Askofu huyo akisema kwamba kanisa linavihitaji vyombo vya habari, haliogopi kumulikwa
kwa kasoro ndani yake na kwamba linahitaji zaidi waumini kutiwa moyo wa kuendelea
kwenye njia ya wongofu. Gazeti hilo lilikuwa linamhoji askofu huyo kuhusu hasa
wajibu wa waandishi wa habari na vyombo vya habari vya kanisa Katoliki na linagusia
hasa muundo mbinu utafutao kusawazisha tamaduni jamii, kitu ambacho kinaonekana kuwaathiri
hata waandishi wakatoliki ambao wanaonekana kuendeleza fedheha na machongelezo licha
ya mema mengi ndani ya Kanisa. Anasema Askofu Martin kwamba kanisa haliogopi kukosolewa,
bali zaidi lina haja ya waandishi wanaowachangamotisha jamii ya waumini kuendelea
kwenye njia ya wongofu, na kwamba kipaumbele cha kwanza cha Kanisa ni kuitangaza habari
njema ya wokovu na kuhakikisha kwamba waumini wanapata malezi bora ya kiimani yaliyo
kamili, matimilifu na ya kweli. Jambo la pili ni kuwaandaa waumini kuishi bila ya
kuitilia shaka imani yao, na kuwajengea uwezo wa kuwa vyombo vya kuipeleka habari
njema ya wokovu pote duniani, bila kuogopa kukumbana na tofauti za kitamaduni na zinginezo,
hata kutoka kwa wale wasio kabisa na imani, huku wakijitahidi kuongoza na kuendeleza
mazungumzo yenye kujenga, katika kutafuta mafao ya wote na ukweli. Hiyo ndiyo maana
ya umissionari wa kanisa, kwani Kanisa kamwe haliwezi kujitenga na ulimwengu kwani
limo ulimwenguni na mazingira ya kiulimwengu yanaliathiri kanisa kama vile yanavyoiathiri
miundo mbinu yoyote ile kwenye jamii. Uinjilishaji hudai kumtangaza wazi kabisa
Kristo na habari njema ya wokovu. Hii ndiyo Kerygma au kiini cha ndani kabisa cha
uinjilishaji kama inavooneakana kwenye mafundisho ya mitume. Bila hilo uinjilishaji
huishia kuwa tendo la kiroho la kibinadamu na wala sio swala la kiroho ndani ya Yesu
Kristo, aliye peke yake Mkombozi aliyekufa na kufufuka kwa ajili ya kumshuhudia Mungu
ambaye ni upendo. Hivyo basi, haya yote yana kuwa na athari juu ya namna kiini cha
Ujumbe wa uinjilishaji, ambacho ni Kristo, ujumbe wa upendo, unatangazwa. Ujumbe huo
hauna budi kuwa kweli ujumbe wa upendo. Askofu mkuu wa Dublin anamshukuru Baba
Mtakatifu Mstaafu Benedicto wa XVI kwa kulisaidia kanisa la Ireland kujenga uhusiano
na maeneo ya malezi ya Ireland ya kizazi kipya. Anaendelea kusema kwamba baba Mtakatifu
Mstaafu Benedikto wa XVI na Baba Mtakatifu wa sasa Franscisko wameonyesha utayari
wa kuzungumza na wanaume na wanawake wanaoishi na kulelewa kwenye tamaduni mamboleo,
jambo ambalo linatia matumaini kwa dunia nzima, kwani uinjilishaji na mazungumzo lazima
viambatane hata kama ni vitu viwili tofauti. Askofu huyo ameutaja mjadala wa hivi
karibuni kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Eugenio Scalfari, mwandishi wa habari
asiyemwamini Mungu wa gazeti maarufu la kila siku nchini Italia kama mfano wa uinjilishaji
mpya, ambao unapaswa kuigwa na uandishi wa Kikatoliki. Amesema hii haimaanishi kufuata
mkumbo bali kuwa na uwezo wa kuonyesha hasa sura halisi ya Kanisa katika ulimwengu
mamboleo.