Ni upendo pekee wa Mungu unaoweza kuziba pengo la maumivu moyoni linaoachwa na maovu
ya binadamu
Msamaha una nguvu ya kipekee inayoweza kumwokoa binadamu na dunia kutokana na dhambi,
na magonjwa mengine ya kimaadili na kiroho. Pia ni upendo peke yake unaoweza kujaza
utupu na pengo ambalo huachwa na matendo maovu kwenye moyo na historia ya mwanadamu.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kwenye mahubiri yake siku ya Jumapili
wakati wa Sala ya Malaika Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu
Petro, Mjini Vatican.
Akigusia masomo ya Jumapili na hasa Injili ya Mtakatifu
Luka 15, papa alielezea kwa kina msamaha wa Mungu unaolinganishwa na hadithi tatu
kwenye injili hiyo. Nazo ni juu ya Kondoo aliyepotea, Shilingi iliyopotea, na ile
ya mwana Mpotevu – ambayo inaonyesha baba na watoto wake wawili, mwana mpotevu, na
yule aliyejifikiria kuhesabiwa haki, kuwa mtakatifu.
Methali zote tatu, anasema
Papa, zinagusia hasa furaha ya Mungu itokanayo na msamaha. Furaha ya Mungu ni kusamehe,
anakazia Baba Mtakatifu Francisko. Ni furaha ya mchungaji anayempata kondoo wake aliyepotea,
furaha ya mama anayeipata shilingi yake iliyokuwwa imepotea, na furaha ya Baba, anampata
mtoto wake aliyekuwa amepotea, aliyekuwa kama mfu, na sasa amepata tena uhai, amerudi
nyumbani.
Ni upendo pekee unaoweza kutoa msamaha wa aina hii na kufurahia
matunda yake, anasema Papa, kwani sio jambo la hisia tu, bali nguvu ya kiroho itokanayo
na Mungu mwenyewe.
Anaendelea kuwa kila mwanadamu anajipata kwenye nafasi ya
yule kondoo aliyepote, ile shillingi iliyopotea, na hata kwenye nafasi ya mwana anayekatalia
mbali uhuru wake halisi wa kuwa mwana mpendwa na kufuata sanamu za uongo, vionjesho
vya furaha, ambavyo vinamfanya kupoteza kila kitu.
Habari njema anayoitangaza
kwa maneno haya Baba Mtakatifu Francisco ni kwamba Mungu hamsahau au kumtupa hata
mmoja wa wana wake wapenzi, kwani Mungu ni Msamaha, na Mungu ni Upendo, ukweli ambao
mwanadamu anaushuhudia kutokana na kujifanya kwake mtu, ndani ya nafsi ya Yesu Kristu.
Japo
Mungu hamsahau mja wake, Mungu huheshimu uhuru wa mtoto wake, huku akimsubiri kwa
mapendo makuu amrudie yeye Baba yake. Naye Mungu aliye mwaminifu humpokea tena kwa
furaha kubwa, kila amrudiaye kwa moyo mkunjufu. Nao moyo wa Mungu hufanya shangwe.
Hata
hivyo, anakazia Baba Mtakatifu kwamba changamoto kubwa ni kwamba mwanadamu hujiona
kuwa mwenye haki daima na kuwahukumu wengine, na hata kumhukumu Mungu mwenyewe. Mwanadamu
anapofikiri kwamba ni jukumu la Mungu kuwaadhibu na kuwahukumu kufa wenye dhambi badala
ya kuwasamehe, anaingia kwenye hatari ya kubaki nje ya nyumba yake Baba, kama alivyofanya
kijana mkubwa kwenye injili ya Jumapili. Badala ya kuingia ndani na kufurahia kurudi
kwa mdogo wake anamkasirikia Baba yake ambaye anamkaribisha na kumfanyia sherehe mdogo
wake.
Anaonya baba Mtakatifu kwamba mwanadamu huenda akakosa fursa ya kuungana
na Mungu kikweli kama anakosa moyo wa huruma, kwani furaha ya msamaha haiwezi kuwa
kwenye moyo usio na huruma, hata kama mhusika anafuata amri zote, kwani ni upendo
tu, unaoweza kuokoa, sio tu kufuata maagizo. Ni mapendo kwa Mungu na kwa jirani ambayo
yanakamilisha amri na sheria zote.
Baba Mtakatifu anawachangamotisha wanaojisikia
kuwa wenye makosa makubwa kwamba hakuna dhambi zisizoweza kusamehewa na Mwenyezi Mungu
na kwamba ni muhimu kukuza moyo wa kuwasamehe wengine ili kuweza kuupokea pia msamaha
utolewao kwa kila mwanadamu.