Vijana wa ulaya wanawataka viongozi wa serikali zao kushirikiana nao kikamilifu kwenye
jitihada za kutafuta suluhisho katika swala la ukosefu wa ajira.
Hili ni ombi
la kundi la vijana 350 wawakilishi wa vijana kutoka nchi mbalimbali za bara la ulaya
waliokusanyika nchini Ubelgiji kwenye mkutano wa vijana ulioandaliwa na bunge la Umoja
wa Ulaya.
Vijana hao wameuomba Umoja wa Ulaya kushirikiana nao kwani wao wanajiona
kama suluhisho la kuaminika kwenye maswala ya kielimu, ukosefu wa fursa za kazi na
maswala mengineyo ya kijamii, ikiwa tu watahusishwa kwenye maisha ya ujenzi wa jamii
na maamuzi ya kisiasa. Nao wamesema wako tayari kuvitumia vipaji vyao vingi na uwezo
wa kufikiria kwenye uvumbuzi na ujasiria mali kwa manufaa ya bara zima la Ulaya.
Kwake
Mgr Omella, Askofu wa jimbo la Calahorra y La Calzada-Logroño (Spain), ukosefu wa
ajira kwa vijana ni donda kwenye soko huria linalosababisha myumbo uchumi. Mons. Omella
alizungumzia juu ya hali ya vijana nchini Uhispania na akasema kwamba kuna umuhimu
wa mbinu mkakati ili kuweza kulitatua tatizo hilo, na hasa katika kutoa elimu ifaayo
hasa kwenye shule za ufundi ili kuwawezesha vijana kuwa na mbinu za kuwasaidia kwenye
kazi au za kuandikwa au za kujiandika wao wenyewe, huku akisema kwamba tendo la vijana
wengine kuacha shule ili kutafuta ajira sio suluhisho kwani elimu ni muhimu katika
utendaji wa kazi za aina yote kwenye jamii.
Naye Sarah Prenger, Mratibu wa
Shirika la Vijana Wafanyakazi Wakristo barani ulaya aliongelea changamoto zinazowakabili
vijana wa ulaya na mikakati iliyopo ya kuwasaidia kuweza kuyamudu maisha yao.
Mengine
yaliyojitokeza kwenye kikao hicho ni pamoja na umuhimu wa kuwategemeza vijana na kuhakikisha
kuna mbinu za ushirikiano kati yao. Mkutano huo pia umezisifu kazi za vijana kote
ulimwenguni na moyo wao wa kujenga utamaduni wa kimataifa. Akiongea kwenye mkutano
huo, Padre Msalesiano wa Don Bosco, Yohanne D’Andrea amesema kwamba swala la elimu
ya kufaa kwa vijana ni swala linalotoka kwenye undani wa moyo, kwani linakumbatia
malezi ya kiutu na kimaadili ya mtu mzima, mwili na roho.
Mkutano huo uliandaliwa
na wanabunge la Ulaya, Patrizia Toia (S&D) na Thomas Mann (EPP) – wakisaidiana na
Konrad-Adenauer-Stiftung, Rete Juventutis, Wasalesiani wa Dono Bosco Ulimwenguni,
na COMECE. Waandalizi wa mkutano huo sasa wanawataka viongozi wa kitaifa, pamoja na
umoja wa ulaya kwa ujumla kuwasikiliza na kuwahusisha vijana kwenye sera na mikakati
ya kuliendeleza bara hilo. Wamewaalika pia vijana kuanzisha juhudi za pamoja kwa ajili
ya kuyakusanya mawazo yao na kuyawasilisha wakati wa uchaguzi wa bunge jipya la ulaya
mwezi Mei 2014.