Siku ya Kimataifa ya Kumuenzi Mwenye Heri Tereza wa Calcutta
Mama Kanisa ana furaha tele kutokana na tendo la Umoja wa Mataifa kuingiza kwenye
kalenda yake, kwa mara ya kwanza kabisa, siku ya Kimataifa ya matendo ya huruma, au
International Day of Charity kwa lugha ya kimwombo. Hii ni siku itakayoadhimishwa
kila mwaka ifikapo tarehe 5 mwezi Septemba.
Askofu mkuu Francis Chullikatt,
Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, anasema kwamba Mama Kanisa
analichukulia tendo hilo kama alama ya kumuenzi Mama Teresia wa Calcutta aliyefariki
dunia mnamo tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1997, na ambaye matendo yake ya huruma yaliugusa
ulimwengu mzima kama ishara ya upendo mkuu wa kujitoa mwenyewe bila ya kujibakiza
kwa ajili ya ndugu zake waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.
Kwa kumuenzi
hivi mama Teresa wa Kalkutta, Mons. Chullikatt anasema kuwa ni ishara ya Umoja wa
mataifa pia kuzithamini kazi za huruma zinazoendeshwa na Kanisa Katoliki kote ulimwenguni
kwa manufaa ya wote wanaosahauliwa na jamii na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.
Askofu
huyo pia amesema kwamba nia ya kanisa katoliki kuonyesha mapendo kupitia matendo ya
huruma ni kumfuasa Kristo mwenyewe aliyejitolea hata kufa juu ya msalaba kwa ajili
ya ndugu zake, na hivyo kuwaonyesha namna ya kupenda wote wenye kumfuasa.
Itakumbukwa
kwamba Mama Teresa wa Calkutta mwenyewe alisema mara nyingi kwamba kazi aliyokuwa
akifanya haikuwa ya kijamii, au Social work, bali ilitokana na maisha ya tafakari
yake ya ndani sana kama mtawa, na iliugusia hasa mwili wa Kristo, ndani ya ndugu zake.
Mama
Teresa alitunukiwa tunu ya Nobeli ya Amani hapo tarehe 11.12.1979, kutokana na kazi
zake za kijasiri na moyo wa mapendo makuu.
Kulingana na Mons. Chullikat kanisa
Katoliki ndilo shirika kubwa zaidi lisilo la kiserikali duniani linalotoa huduma nyingi
zaidi hasa za kielimu na kiafya. Zaidi ya asilimia 26 ya huduma zote za kiafya duniani
hutolewa na Kanisa Katoliki. Naye mama kanisa hutoa huduma hizo sio kama sehemu ya
kazi za kijamii, bali kama sehemu ya kazi zake za kichungaji zinazotokana na mapendo
ya Kikristo yabubujikayo kutoka moyoni na yanayowakumbatia wengine kama zawadi kutoka
kwa mwenyezi Mungu.