Baraza la Mabaraza ya Makanisa ya Ulaya pamoja na Baraza la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Ulaya yamewaomba waumini wote wa ulaya kuungana pamoja na Baba Mtakatifu francisko
kuombea amani Syria, Mashariki ya kati na kote duniani hapo siku ya Jumamosi (07/09/2013).
Mabaraza hayo pia yamewaalika viongozi wa mataifa 20, (G20) wanaoendelea na
mkutano wao wa mwaka mjini Petersburg, Urusi , kujiunga na Askofu mkuu wa Kianglikani
wa Canterbury, Justin Welby, na Baba Mtakatifu Francisco na viongozi wengine wa Kikanisa
kufikiria kwanza njia ya majadiliano wala sio silaha, katika kukabiliana na changamoto
zinazoikabili dunia ya leo.
Kwenye ujumbe wa pamoja kuhusiana na migogoro na
kinzani ya kivita inayoendelea nchini Syria, Mabaraza haya mawili ya makanisa ya Kikristo
barani ulaya yanapinga aina yoyote ya vita na yanaonyesha mshikamano wao na wa makanisa
ya ulaya na wakristo na watu wote wanaoendelea kuteseka nchini Syria kutokana na mauaji
ya halaiki kwenye vita vinavyoendelea nchini humo.
Maaskofu hao wanasema kwamba
amani ya kweli hutoka kwake mwenyezi Mungu na hivyo ni vyema kumwomba Mungu atujalie
amani ndani ya mioyo yetu na kwa wale walioathirika na vita.
Ujumbe huo umewekwa
sahihi na Kardinali Peter Erdò, Askofu Mkuu wa Esztergom, Budapest, aliye pia rais
wa Baraza la mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Ulaya; na Christopher Hill, Askofu wa
Kianglikani wa Guildford, na rais wa Baraza la makanisa Ulaya.