Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) linawataka wafuasi wake kujiunga na kampeni ya
kimataifa kwa ajili ya kusitisha ufisadi, dhambi ambayo inawaathiri hasa maskini.
Takwimu zinaonesha kwamba kila mwaka zaidi ya dolla trilioni moja za kimarekani hupotea
kutokana na rushwa, ufisadi na ukwepaji wa kodi.
Kampeni ya kimataifa dhidi
ya ufisadi imepanga matukio kadhaa kwa ajili ya wiki ya tarehe 14 hadi 20 Octoba 2013.
Mwito huu ambao umepewa jina Exposed 2013, utawahamasisha watu kote duniani dhidi
ya uovu wa ufisadi. Kampeni hii inaongozwa na kundi la wakristo lijulikanalo kama
Micah Challenge International. Jina la kundi hili linatokana na kifungu cha Mika 6:8
– “Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu
na Mungu wako!”
Kampeni hii inatarajia kuandaa vigilia ya zaidi ya 2000 sehemu
mbalimbali za dunia kwa ajili ya watu maskini. Mbali na vijilia, kikundi cha Micah
Challenge International kinatarajia kukusanya sahihi milioni moja wakati wa kampeni
hiyo na kuwasilisha sahihi zingine milioni moja kwenye mkutano mkuu wa nchi maskini
duniani au G20 utakaofanyika mwezi Novembar 2014.
Naye katibu mkuu wa Baraza
la Makanisa Kasisi Olav Fyske Tveit anasema kwamba Baraza la Makanisa Ulimwenguni
limeamua kujihusisha na kampeni hii kwa kufuata mwito wa Mungu wa kuwapendelea na
kuwa karibu zaidi na watu maskini. Kasisi Olav Fyske Tveit anasema kwamba ufisadi
unaendelezwa na miundo mbinu ya kiuchumi, kitamaduni na kimaadili ambayo inaongozwa
na ubinafsi na uchu wa mali, na utajiri wa haraka. Pia makundi ya kisiasa na hata
viongozi na watu binafsi wanao mchango wao katika kuendeleza ufisadi kwenye jamii.
Hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kwenye juhudi za kuipinga miundo mbinu hiyo
ambayo inaendeleza unyanyasaji wa watu wengi, na kwamba ni katika kuishika haki ya
kiMungu tu dunia itakapoweza kukabiliana vilivyo na donda sugu la ufisadi. Amesema
Kasisi Tveit kwamba Exposed 2013 ni juhudi muhimu inayoenda sambamba na jitihada za
Baraza la Makanisa la kuwa karibu na makanisa mahalia kwenye jitihada zao za kuupinga
unyanyasaji wa kiuchumi. Malengo ya kampeni ya Exposed 2013 pia yanalingana na mada
ya mkutano mkuu ujao wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, utakaofanyika mjini Busan,
Jamhuri ya Korea mnamo October 30, 2013 hadi Novemba 8, 2013. Programu ya Baraza
la Makanisa Ulimwenguni inayoshughulikia maswala yanayohusiana na umaskini, mali na
Mazingira hushughulikia pia biashara inayozingatia haki, unyanyasaji wa kiuchumi,
heshima kazini, na maadili ndani ya dunia ya utandawazi.