Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya Kichungaji kwenye mji asili wa Mtakatifu
Francisko wa Assisi wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko hapo tarehe
4 Octoba mwaka 2013. Papa alilichagua jina la Mtakatifu huyu alipoteuliwa kuwa Khalifa
wa Mtakatifu Petro hapo tarehe 19 Machi mwaka 2012.
Atakapowasili Assisi baba
Mtakatifu atapokelewa na Askofu Mkuu wa Assisi, Mons. Domenico Sorrentino na wawakilishi
kadhaa wa serikali ya Italia. Baadhi ya shughuli za kichungaji atakazokamilisha akiwa
Assisi ni pamoja na kukitembelea kituo cha watoto walemavu cha Serafico na kile cha
watu maskini cha Mtakatifu Francisko ambapo atakutana maskini wanaosaidiwa na shirika
la misaada la kanisa Katoliki, Caritas. Katika hija yake, Papa Francisko ataadhimisha
ibada ya Misa Takatifu sehemu mbalimbali, pamoja na kuyatembelea maeneo ya kihistoria
ya mji huo kama vile Kanisa la Mtakatifu Damiano ambapo inasemekana ndipo Francisko
alipaopata wito wake kwa mara ya Kwanza pale Yesu alipomtokea na kumwuomba aende akamjengee
nyumba yake. Papa atayatembelea pia makanisa makuu ya Mtakatifu Clara na Mtakatifu
Rufino, na madhabahu ya Rivotorto pamoja na “jela” chumba alichokuwa anatumia Mtakatifu
Francisko kwa sala zake baada ya safari zake za kuihubiri injili huku na huko. Papa
pia atakuwa na mikutano ya hadhara na ya faragha na watu mbalimbali kama inavyo onyesha
ratiba ya hija ya Papa Assisi iliyotolewa na Vatikani mwanzoni mwa wiki.