2013-09-05 11:17:54

Kukubali mwaliko wa Papa Francisko kwa ajili ya amani, ni mwako mpya kiroho


Mwamko mpya wa kiroho unajionesha kwenye ombi la Baba Mtakatifu la kufunga na kusali kwa ajili ya kuomba amani. Ombi hilo pia linaonyesha umoja wa Kanisa ulimwenguni kwa mwuungano huo wa matendo ya sala maalum pote duniani. Ni maneno yake Salvatore Martinez raisi wa kitaifa wa kikundi cha mwamko wa kiroho cha Charismatic, nchini Italia.

Anasema rais huyo kwamba hapo siku ya Jumamosi tarehe saba Septemba 2013, makundi na jumuiya 1900 za mwamsho wa kiroho yatajumuika pamoja na Papa Francisko kwenye mafungo na maombi, kwa nia ya kujenga ukuta wa moto, ukuta wa upendo, (maneno ya Mtakatifu Katarina), ukuta mkubwa wa sala uliojengwa kwa mawe yaishiyo ya wanaume na wanawake wa sala.

Amesema Salvatore Martinez kwamba hata kama kwenye dunia ya leo kuna mwonekano wa ukosefu wa sala, wao wanaamini na kuungama kwamba sala ni muhimu sio tu kwa kutusaidia kufungua mioyo, bali hata kwa kufungua akili za wanadamu ili waweze kukumbatia lengo la kujenga jamii kwa manufaa ya watu wote, na kwamba ni yule tu mwenye kusali anayetambua jinsi jirani yake alivyo zawadi kutoka kwa Mungu na sio shida ya kutatuliwa au adui wa kupigwa.

Anasema ni mwanamke au mwanamume mwenye kusali tu awezaye kuwa na tumaini na hekima hapa duniani, na awezaye kuwa mjumbe wa upendona amani, ambayo ni mapaji yatokaye kwake Mungu. Ni hao tu wanaoweza kutetea na kulinda maisha na maadili yanayounganisha wanadamu kama vile msamaha, ukweli, haki na amani, ili kuweza kujenga udugu unaozikumbatia nchi, watu, dini, rangi, tamaduni na kabila mbalimbali.

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana Jumapili iliyopita (01/09/2013) Baba Mtakatifu Francisko alionyesha uchungu wake kutokana na hali ya mateso inayowakumba wananchi wa Syria kwenye mapigano yanayoendelea nchini humo. Kutokana na hayo aliomba siku ya kufunga na sala ili kuomba amani kwa ajili ya Syria, Mashariki ya kati, na ulimwenguni kwa jumla.

Papa pia aliwaalika watu wote wenye mapenzi mema, Wakristo na wasio wakristo, na kukutana kuanzia saa moja jioni hadi saa sita usiku kwenye uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatikani kwa ajili ya sala pamoja.











All the contents on this site are copyrighted ©.