Mwaliko maalum wa kuombea amani Mashariki ya kati.
Wakristo duniani kote wanaalikwa hapo Jumamosi tarehe saba (07.09.2013) kuwaombea
waathirika wa vita na migogoro inayoendelea huko Syria na nchi nyingine za Mashariki
ya kati. Ni mwaliko uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika
wa Bwana siku ya Jumapili alipokutana na kusali na maelfu ya waumini kutoka sehemu
mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu ameiomba jumuiya ya waumini, kupitia kwa Mama
Bikira Maria, Malkia wa Amani, kusali, kufunga na kujinyima kwa ajili ya nchi ya Syria
na mashariki ya kati kwa jumla.
Na hapa jijini vatikani, siku hiyo ya tarehe
7, kwenye uwanja wa kanisa kuu la Mt. Petro, kuanzia saa moja jioni hadi saa sita
usiku (kwa majira ya kiitalia) waumini watakusanyika na kuunganika kwa sala, moyo
wa toba na makesha maalum kwa nia hiyo ya kuomba amani Syria, Mashariki ya kati na
kote duniani.
Akitoa mwito huo, Papa Fransisco amesema kwamba dunia inahitaji
kuona vitendo vya mshikamano wa sala na kusikia maneno ya kutia moyo na yenye kuleta
amani.
Makanisa mahalia na watu wote wenye mapenzi mema wameombwa kuandaa
mikutano ya sala siku hiyo ya tarehe 7 Septemba ambayo ni siku ya vigilia ya kuzaliwa
kwake mama Bikira Maria, inayoadhimishwa na Mama kanisa kila mwaka ifikapo tarehe
8 Septemba. Ni mwaliko kumwomba Mama huyu aliye Malkia wa Amani kuisaidia dunia kujenga
kila siku, utamaduni wa amani na mazingira ya amani yaliyo muhimu kwa mafao ya watu
wote duniani.